Wananchi katika Manispaa ya Iringa wameshauriwa kujenga vyoo bora vya gharama nafuu ili kuweza kutunza afya zao na kuepuka adha ya kutokuwa na vyoo na kuwekewa bendera nyekundu katika kaya zao.
Kauli hiyo imetolewa na Meya wa Manispaa ya Iringa Mheshimiwa Alex Kimbe katika hafla fupi ya kukabidhiwa choo bora cha gharama nafuu kutoka kwa Meneja wa Mradi wa ACRA, mradi wa Usafi Iringa bwana Joerg Henkel kilichojengwa mtaa wa Igeleke katika kata ya Mkimbizi.
Amesema choo hicho kilichojengwa eneo la makaburi mapya ya Igeleke,ni choo kwaajili ya matumizi ya jamii hasa ya wananchi wanaokuja kufanya shughuli za mazishi katika makaburi hayo, hivyo amewaomba wataalam wa Manispaa na watendaji wa Kata nyingine kuiga mfano wa vyoo hivyo ili kuwasaidia wananchi wasio na vyoo bora katika kata zao wajenge vyoo hivyo bora vya gharama nafuu.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa choo hicho mtendaji wa kata ya Mkimbizi Bwana Mlole Ndwada amesema choo hicho kimegharimu kiasi cha shilingi 719,000/= ambapo kata imechangia gharama ya shilingi 92,000/= na mfadhili ambaye ni mradi wa Usafi Iringa amechangia kiasi cha shilingi 627,000/=.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Diwani wa Kata ya Mkimbizi MheshimiwaSeverin Mtitu watendaji wa kata ya Mkimbizi wananchi pamoja na wafanyakazi kutoka mradi wa ACRA.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa