Baraza la Madiwani Manispaa ya Iringa chini ya Mwenyekiti Mstahiki Meya Mhe. Ibrahim Ngwada leo tarehe 6/5/2021 limefanya ziara ya robo ya tatu (Januari-machi 2021) ya kutembelea na kukagua miradi inayotekelezwa na Manispaa kwa lengo la kuona mafanikio na changamoto zilizopo katika miradi hiyo
Akiongea katika ziara hiyo Mhe. Ngwada amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri Hamid Njovu pamoja na wataalam kwa kujenga miradi mingi ya maendeleo kwani itatatua changamoto za wananchi katika Sekta ya Afya,Elimu,Maji na zingine
Aidha Mhe. Ngwada amewapongeza wadau mbalimbali waliojitokeza kutoa misaada ya fedha na vifaa vya ujenzi kuhakikisha miradi hiyo inakamilika na kunufaisha wananchi wa Manispaa
Amesema wadau walioifadhili Halmashauri kufikia malengo hayo ni pamoja na Kampuni ya ASAS DAIRIES na IRUWASA na kuwashukuru kwa msaada mkubwa walioutoa katika Manispaa ya Iringa
Miradi iliyotembelewa na kukaguliwa ni pamoja na Ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Kigungawe, Ujenzi wa Jengo la Utawala stendi mpya lgumbilo, Ujenzi wa Bweni na Maabara shule ya Sekondari Mawelewele na ujenzi wa Bwalo shule ya Sekondari Kwakilosa na Mingineyo
Aidha Ngwada amewataka wataalamu kutumia vizuri fedha ili thamani ya miradi iendane na fedha iliyotolewa pia kuhakikisha miradi hiyo inakuwa na ubora uliokusudiwa pia amesema ipo haja ya kuwepo na ziara ya kukagua na kutembelea miradi ya maendeleo kila robo (kila baada ya miezi mitatu) kwani itasaidia kuhamasisha utendaji wa kazi na kuleta msukumo wa ukamilishaji wa miradi kwa wakati
Mh. Eliud Mvela ni mjumbe wa Baraza la Madiwani ametoa rai kwa wataalamu kufanya kazi kwa weledi kwani wameaminiwa na Serikali kutumia taaluma zao katika kuiletea Halmashauri Maendeleo, pia ameagiza wasimamizi wa miradi inayosuasua kuhakikisha inakamilishwa kwa wakati uliopangwa
Kwa upande wake Naibu Meya wa Manispaa Mhe, Kenyata Likotiko amewataka wataalamu kuwashirikisha wanachi kuanzia mwanzo wakati ujenzi unaanza ili waweze kuchangia nguvu zao kwani kwa kufanya hivyo itaondoa malalamiko. Kwa wananchi kutokushirikiswa katika miradi inayotekelezwa
Hamid Njovu Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa amesema ameshukuru Baraza kupokea Miradi hiyo na kuahidi kutoa ushirikiano zaidi katika umaliziaji wa ujenzi wa miradi hiyo kwa manufaa ya wananchi.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa