Shule ya Msingi Uyole iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imepokea jumla ya madawati 50 kutoka benki ya CRDB kama sehemu ya kurudisha fadhila kwa jamii.
Akizungumza katika halfa fupi ya makabidhiano ya Madawati hayo, iliyofanyika Shuleni hapo, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Mhe. Ibrahim Ngwada amesema kuwa anawashukuru wadau hao kwa mchango wa madawati kwani utasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua tatizo la upungufu wa madawati lililopo shuleni hapo.
" Lengo la benki sio kufanya biashara zake tu, bali pia kusaidia jamii iliyopo. Kwa niaba ya Wanairinga na Halmashauri nawashukuru sana kwa msaada wa madawati mlioutoa kwetu. Shule hii ni mpya na ya kisasa imegharimu zaidi ya Tsh. Milioni 300. Tumechonga madawati 105 na meza 30. Tulitarajia kusajili wanafunzi 315, lakini mpaka sasa walioandikishwa ni 460. Hivyo kutokana na ongezeko la wanafunzi, tumekuwa na upungufu wa madawati". Amesema Ngwada.
Aidha, Meneja wa CRDB Kanda ya kati, Ndg. Chabu Mishwamo amesema kuwa wao kama wadau wakubwa wa serikali wana wajibu wa kuchangia katika shughuli mbalimbali za kijamii na kuungana na kuisaidia Serikali ambayo imefanya kazi kubwa sana ya kujenga madarasa mengi nchini Tanzania.
" Tumekuja mahali hapa Uyole kwa ajili ya kuleta madawati, Sisi kama wadau tuna wajibu wa kuangalia ni kwa namna gani tunasaidia Serikali kwa ajili ya kujenga Taifa bora hapo baadae, kwa mahali hapa tumeleta madawati 50 ambayo yataleta tija na chachu kwa wanafunzi wetu kuhudhuria darasani na kuketi, kujifunza na kuwa wazalendo". Amesema Mishwamo.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Ndg. Justine Sanga ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa Shule hiyo ya Uyole kwani imesogeza huduma na imesaidia kupunguza ajali kwa wanafunzi waliokuwa wakisafiri umbali mrefu.
Aidha Sanga ameishukuru Benki ya CRDB kwa msaada wa madawati hayo, kwani bado shule ilikuwa na uhitaji.
Awali akisoma taarifa fupi ya shule hiyo Mwalimu Mkuu Ndg.J oseph Millinga amesema, Shule ya Uyole ilijengwa kwa ajili ya kupunguza msongamano wa wanafunzi uliokuwa katika Shule ya Msingi Kitwiru, pia ilijengwa ili kupunguza ajali za wanafunzi waliokuwa wanasafiri umbali mrefu. Shule ilifunguliwa rasmi mwezi Januari, 2024 kwa usajili wa wanafunzi waliohamia 306. Mpaka sasa imesajili zaidi ya wanafunzi 400.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa