Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Ndg. Kastori Msigala amewaonya Maafisa Maendeleo ya jamii wa Manispaa ya Iringa kutojihusisha na utoaji wa mikopo hewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na makundi maalumu kwani wakifanya hivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Msigala ameyasema hayo katika Ukumbi wa Manispaa ya Iringa wakati akifungua Mafunzo ya Muongozo Mpya wa Usimamizi na Utoaji Mikopo ya Vikundi vya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu ambayo yametolewa kwa Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii kwa lengo la kuwajengea uwezo ili wakatoe elimu kwa wanufaika wa mikopo kwenye Kata zao kwani zaidi ya Fedha kiasi cha Shilingi Milioni 800 za Kitanzania zimetolewa na Halmashauri ya Iringa kwa mwaka wa fedha 2024/25 kwa ajili ya mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
"Lengo la Serikali ni kuendelea kutoa tija na ufanisi katika zoezi zima la kutoa mikopo ya wanawake, vijana na makundi maalumu, nataraji mafunzo haya yatatoa muongozo mpya kwenu juu ya usimamizi wa utoaji wa mikopo kwa wataalamu wetu pindi tutakapoanza kutoa fedha upya ili changamoto zile za nyuma zisijitokeze tena, Nawaomba mkafanye kazi ya utoaji wa mikopo kwa uadilifu mkubwa sitegemei kusikia habari za vikundi na mikopo hewa. Watakaojihusisha na hili sitawavumilia, watachukuliwa hatua." Amesema Msigala.
Afisa Maendeleo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ndg. Saida Mgeni amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo Maafisa Maendeleo ya Jamii kama wasimamizi wa mikopo hiyo kwenye Kata ili kupata maelekezo kutoka Serikalini kuhusiana na Muongozo, Kanuni pamoja na Sheria za Utoaji wa mikopo na hatimaye kutatua changamoto za mikopo ambayo haikurejeshwa kwa wakati, hivyo matarajio ya Serikali ni kuwa mikopo inayoenda kutolewa mwaka huu itafuta changamoto au mapungufu mbalimbali yaliyojitokeza katika urejeshaji wa mikopo.
Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Iringa, Ndg. Mwatumu Dossi amesema kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuboresha utoaji na ufuatiliaji wa mikopo hiyo kwani awali vikundi vimekuwa vikifanya udanganyifu, vingine vimekuwa vikisambaratika na kushindwa kurejesha mikopo ambayo walichukua, hivyo sheria na kanuni za sasa zitawabana.
Aidha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Ndg. Kastori Msigala amewakumbusha maafisa hao kushiriki katika Zoezi la Uandikishaji litakaloanza Tarehe 11 mpaka 20 Novemba, 2024 na hatimaye kujitokeza kwa wingi kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaohusisha Wajumbe wa Mtaa na Mwenyekiti wa Mtaa ambao utafanyika Siku ya Tarehe 27 Novemba, 2024.
Tayari umma umeshataarifiwa kuhusiana na taratibu za maombi na sifa za wanufaika wa mikopo hiyo mara tu mafunzo hayo yatakapokamilika taratibu nyingine zitafuata.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa