MKUU wa wilaya ya Iringa Mohamed Moyo amewaongoza watalaamu na viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kwenda mjini Morogoro kujifunza namna nzuri ya kuwapanga wafanyabiashara ndogo ndogo ( Machinga) katika maeneo yao .
Ziara hiyo iliyofanyika hivi karibuni ni sehemu ya maandalizi ya Utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan juu ya Halmashauri zote kuwapanga machinga kwenye maeneo sahihi .
Ziara hiyo imeongozwa na mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe.Mohamed Moyo,akiwa ameambatana na Mstahiki Meya na Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Mkurugenzi,Madiwani, Mwenyekiti wa CCM Wilaya na wataalamu kutoka Idara mbalimbali.
Akizungumzia lengo la ziara hiyo Moyo alisema ni kupata mafunzo ya namna wenzao walivyofanikiwa kuwaondoa machinga kwenye barabara,mitaro na kuwapatia sehemu rasmi ya kufanyia biashara zao.
Moyo alisema kwenye ziara hiyo wamepata somo kubwa,wakirudi Iringa watakaa na kutafakari, na kuyatendea kazi waliyojifunza kwa kuwashirikisha na kuwapatia maeneo ya kufanya biashara machinga wa wilaya yao na kuhakikisha maagizo ya Mhe Rais wanayatekekeza kwa usalama na utulivu bila ya fujo yoyote.
"Kweli ni niupongeze uongozi mzima wa Morogoro,wameweka mawazo yao pamoja mpaka kufanikiwa kwa machinga kuwa kwenye maeneo mazuri,na jinsi gani wataalamu wanavyo shirikiana na machinga,zaidi Mambo yamekuwa shwari hapa Wilaya ya Morogoro,"alisema Moyo.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa mhe: Ibrahim Ngwada, alisema wamepata fursa ya kutembelea vyanzo vingine vya mapato vya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ikiwemo ukumbi wa community center ambao kwa sasa umeboreshwa sana.
"Sisi pia tunalo eneo la Maendeleo la community center,ambalo nia yetu ni kuliboresha,kweli wametufundisha na kuweza kuona namna community center ipo na inavyowasaidia kuingiza mapato ya Halmashauri,"alisema Mhe. Ngwada.
Alisema wamejifunza jambo kubwa baada ya kutembelea stendi ndogo ya Morogoro kwani wamehamishia baadhi ya vitengo katika eneo hilo,hivyo wamepata mawazo na wataenda kutafanyia kazi katika Halmashauri yao.
"Kikubwa niseme tumekuja Morogoro na ziara yetu imekuwa na mafanikio na tumejifunza zaidi,"amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iringa Manispaa Said Rubeya alisema wamejifunza jinsi gani ya kushughulikia wafanyabiashara wadogo ambao wengi ni vijana wao bila ya kuwaumiza.
Kaimu mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa Omary Mkangama alisema watakwenda kutekeleza agizo la mhe Rais Samia kwanza kwa kupeleka mawazo katika vikao vya kisheria na kufuata taratibu zote ikiwemo kuwashirikisha wafanyahiashara ndogo ndogo azma ya kutekeleza agizo la Rais
Naye Michael Walusi kaimu mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro,alisema ziara ya viongozi hao kutoka Wilaya ya Iringa ni muendelezo wa Manispaa ya Morogoro kupokea wageni ambao wanakuja kwa ajili ya kujifunza namna walivyofanikiwa kuwaondoa wajasiriamali wadogo wadogo na Machinga ambao waliokuwa wametapakaa maeneo mbalimbali na kufanya biashara zao bila utaratibu.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa