Na Mwandishi Wetu, Iringa
MKUU wa Wilaya ya Iringa, Mohamed Moyo, amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari zinazotolewa na wataalam wa afya kufuatia kuibuka kwa wimbi la nne la ugonjwa wa Corona.
Alisema hayo leo (Disemba 7, 2021) wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kata za Mshindo na Miyombo-Kitanzini ambao pia uliohudhuriwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Mhe.Ibrahim Ngwada na mhe Epautwa Maadhi ukiwa na lengo la kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.
Moyo alisema wakati wakiendelea kuchukua tahadhari la wimbi hilo ambalo lilianza kujitokea mwishoni mwa Oktoba mwaka huu, wananchi waendelee pia kujitokeza kupata chanjo ambazo zinatolewa bure kwenye vituo vya afya wilayani humo.
Aidha, Mkuu wa Wilaya amewapongeza waheshimiwa madiwani kwa jinsi wanavyoendelea kusimamia miradi ya ujenzi wa shule za sekondari na vituo vya afya inayojengwa chini ya fedha za UVIKO-19 zilizotolewa na Serikali kuu.
Kuhusu sensa ya watu na makazi inayotarajia kufanyika mwakani 2022, Mkuu wa Wilaya amewataka wananchi kuwapa ushirikiano makarani wa Serikali ili kupata takwimu na ifikapo muda huo watu wote wanapaswa kuwa katika makazi yao husika.
Kwa upande wake Mstahiki Meya Manispaa ya Iringa, Mhe. Ngwada, alimweleza Mkuu wa Wilaya kuwa Manispaa hiyo inatekeleza miradi ya UVIKO-19 kwa kujenga madarsa 33 na kituo cha afya cha kisasa cha Mkimbizi katika kata ya Mkimbizi ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika kata ya Mtwivila.
Mhe.Ngwada alisema Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, pia ina mpango wa kuboresha ujenzi wa jengo la Community Centre.
Aliongeza kuwa halmashauri pia itahakikisha miradi yote inayojengwa kwa fedha za ndani kama vile ujenzi wa soko la Mlandege na stendi ya Igumbilo inakamilika kwa wakati.
"Mhe Mkuu Wilaya lengo letu tunataka kuhakikisha kuwa halmashauri yetu ya Manispaa ya Iringa inakuwa ya mfano," alisema Mhe.Ngwada.
Nao wananchi waliwasilisha kero zao kwa viongozi hao ambapo Agustino Sambaji alisema kumekuwa kero ya maji kwa wasomaji wa mita kuongeza idadi ya namba za mita na kuleta changamoto kwani gharama zinazokuja ni kubwa mno ukilinganisha na matumizi ya maji wanayotumia wananchi.
Sambaji pia alizungumzia suala la kupanda kwa bei pembejeo kama mbolea hali ambayo imesababisha kilimo msimu huu kuwa kigumu.
Kwa upande wake Shabani Borakupata mjumbe wa Kitanzini amesema miundo mbinu bado ni tatizo kwani barabara zimekuwa ni mbovu na kuwa kero kwa wananchi na kuiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuzijenga kwa kiwango cha lami.
Akijibu kero zilizotolewa na wananchi hao, Mkuu wa Wilaya alisema kero zote Serikali imezichukuwa na kuwaahidi kuwa itazifanyia kazi.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa