Mkuu wa wilaya ya Iringa Mhe. Kheri James ametoa wito kwa wafanyabiashara wadogo (Machinga) kuwa na umoja ili kuepuka makundi yanayoathiri malengo ya biashara.
Ameyasema hayo, akiwa kwenye mkutano na wafanyabiashara wadogo (Machinga) uliofanyika Aprili 5, 2024 katika Soko la Mlandege lilipo mjini Iringa kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali zinazowakumba wafanyabiashara hao.
"Tukiweka Simba, tukiweka Yanga, tukiweka CCM, tukiweka CHADEMA, tukiweka TLP tutauza vingapi? Matokeo yake vile ambavyo sio kipaumbele na lengo letu vinabeba nafasi kubwa kuliko lengo la biashara ambalo limetutoa nyumbani kuja kazini. Matokeo yake makundi yale yanaathiri mpaka mazingira ya biashara, maamuzi ya biashara na yanaleta mpasuko miongoni mwenu na kushindwa kudai haki zenu". Amesema DC Kheri
Aidha, Mhe. Kheri amewashauri wafanyabiashara kuliko kulumbana wenyewe kwa wenyewe ni vyema kujikita katika kutoa maoni yenye tija kwa serikali juu ya kuboresha zaidi biashara zao. Vilevile, amewaasa wafanyabiashara hao kukaa katika maeneo waliyopangiwa ili kuepusha migongano kati yao na Askari wa Manispaa.
Wakati huo huo, wafanyabiashara hao wametoa rai kwa serikali kuwasogezea huduma kama vile kituo cha dalala au bajaji, mama lishe pamoja na soko la vyakula kwa ajili ya kuvuta wateja kuweza kufika maeneo ya soko hilo na kununua bidhaa zao.
Mhe. Kheri ameahidi kushughulikia Kero zilizotolewa na wafanyabiashara hao ndani ya siku saba ili kuweza kutoa suluhisho la changamoto hizo.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa