Ikiwa ni muendelezo wa Kampeni ya usafi ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Mkuu wa Wilaya ya Iringa Komred Kheri James amewapongeza Wananchi na Viongozi wa Manispaa hiyo kwa usimamizi bora wa usafi wa mji.
Komred Kheri James ameyasema hayo leo Machi 30, 2024 katika Kampeni ya usafi wa mwisho wa mwezi iliyofanyika katika Kata ya Kihesa Manispaa ya Iringa.
Akizungumza katika Kampeni hiyo Komred Kheri ameeleza kuwa Manispaa na viunga vyake imekuwa na mazingira safi kutokana na mpango mzuri wa usafi unaoshirikisha wananchi kikamilifu kwa kushiriki na kuchangia gharama za usafi wa maeneo yao ya huduma na makazi.
“Niwapongeze Mkurugenzi na wataalamu kwa namna ambavyo mipango ya usafi ya mji wetu inatekelezwa vizuri hivyo niwaahidi nikiwa kama Mkuu wa Wilaya nitaendeleza yale yote mazuri mliyoanza na hata mkiniamsha saa 8 usiku kwa kazi hii tutaifanya ili kuhakikisha Manispaa yetu ya Iringa inakuwa safi, hasa tukianza kwa kutokufanya biashara katika maeneo ambayo hayajapangwa na serikali” Amesema DC Kheri
Kupitia Kampeni hiyo Komred Kheri amewasihi wananchi kuendelea kutekeleza Kampeni hii ya usafi katika maeneo yao ili kudhibiti mlipuko wa maradhi, kuweka vizuri mandhari ya mji ili kuepuka usumbufu unaoweza kutokana na takataka kuzagaa.
“Kampeni hii ya usafi ina dhima maalum ya kuhakikisha mji wetu unakuwa safi, kupambana na magonjwa ya mlipuko, kuweka vizuri mazingira yetu ya biashara na hudumu na mwisho usafi ni kwaajili yetu sisi wenyewe, niwaombe wananchi leo tumeshiriki hapa Kihesa lakini hili ni tangazo na hamasa kwa kila mmoja kufanya usafi katika eneo lake” Amesema DC Kheri
Pamoja na kuwahimiza wananchi kufanya usafi na kulipia gharama za usafi, Komred amewataka Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata na Mitaa kuongeza kasi ya usimamizi ili kuongeza uwajibikaji wa kila mdau katika kuhakikisha maeneo yanakuwa safi na salama.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Mhe. Ibrahim Ngwada ametumia fursa hiyo kumkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Iringa na kuwaomba wananchi wa Iringa kuendelea kudumisha suala la usafi katika meneo yetu ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa
“Sisi kama Halmahsuri tumekubali na tunaingia gharama kubwa kila siku tunatumia mafuta zaidi ya Lita 350 mpaka 400 kwajili ya usafi, tunao vibarua zaidi ya 50 kwaajili ya kufanya usafi wanaozunguka ndani ya Manispaa na kuwalipa mishahara na kununua vifaa, nikuombe Mkuu wa Wilaya uendelee kuhimiza tozo za usafi kwa wananchi Majumbani, Nyumba za wageni (Guest Houses), Mashuleni na Taasisi zetu ili mji wetu uendelee kuwa msafi zaidi kama ambavyo huwa tunashika nafasi ya 1 au 2 kwa Halmashauri za Manispaa” Amesema Mhe. Ngwada
Kampeni hiyo ya usafi kwa Manispaa ya Iringa yenye kaulimbiu ya “Usafi wa Mji Wetu ni Wajibu Wetu” imehudhuriwa pia na Viongozi, Watendaji na Watumishi wa Kada zote.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa