Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Frelimo mkoani Iringa Dkt. Hassan Mtani amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kiasi cha Tsh. Milioni 247,935,760 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya watoto, kukamilisha miundombinu na kuongeza bajeti ya vifaa tiba ili kuweza kupunguza idadi wa vifo vya mama na mtoto.
Hayo yamebainishwa na mganga mfawidhi wa Hospitali ya Frelimo Dkt. Hassan Mtani wakati akitoa taarifa kwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mhe. Abood Mohamed Abood ambae pia ni mlezi wa CCM Mkoa wa Iringa, alipotembelea hospitalini hapo siku ya madhimisho ya miaka 47 ya kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Kwa mwaka 2022 akina mama 700 waliojifungua katika hospitali yetu kati yao kifo kilichotokea kilikuwa ni kimoja tu ambacho kilitokana na kifafa cha mimba, vifo vimepungua ukilinganisha na kipindi cha nyuma”. Amesema Dkt. Hassan
Dkt. Hassan aliongeza kwa kusema lengo la kuanzishwa kwa hospitali hiyo ni kupunguza vifo vya mama na mtoto vilivyokuwa vinatokea wakati wa kujifungua pamoja na kupunguza msongamano katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kutokana na kusogeza huduma karibu na wananchi.
Akizungumza na watumishi katika hosptali hiyo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mhe. Abood Mohamed Abood amewahimiza watumishi wa afya kuzingatia weledi, maadili na viapo vyao katika utoaji wa huduma za afya.
Abood amesema serikali inatambua changamoto ya uhaba wa watumishi wa afya kama ilivyoelezwa na mganga mfawidhi, hivyo amewataka watumishi waliopo kuwahudumia wananchi kwa weledi wakati serikali ikiendelea kuongeza watumishi katika sekta hiyo na kuboresha miundombinu yote ya afya kwa kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa