Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Mhe. Ibrahim A. Ngwada amezindua rasmi kliniki ya ardhi kwa lengo la kusikiliza na kutatua migogoro mbalimbali ya ardhi kwa wananchi wa Kata ya Nduli iliyopo Manispaa ya Iringa.
Uzinduzi huo, umefanyika katika Ofisi ya Kata hiyo kwa lengo la kusikiliza migogoro mbalimbali ya wananchi huku akiambatana na Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali wakiwemo Katibu Tawala wa Wilaya ya Iringa, Ndg. Michael Semindu, Katibu wa CCM Wilaya Ndg. Hassan Makoba, Diwani wa Kata ya Nduli Mhe. Bashiri Mtove, Diwani Viti Maalum Mhe. Paskalina Lweve, Wataalamu wa ardhi Mkoa na Manispaa, Wakuu wa Idara na Vitengo, Watendaji wa Kata na Mitaa, Afisa Tarafa, Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na wananchi wa Nduli.
Ngwada amesema kuwa Mkutano huo ni matokeo ya ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mhe. Kheri James iliofanyika Mei 31, 2024 kwa ajili ya ukaguzi wa miradi na kusikiliza wananchi ambapo baada ya kufika Kata ya Nduli migogoro mingi ya ardhi iliibuka.
Aidha Ngwada amesema kutokana na hali hiyo ilipelekea Mkuu wa Wilaya kutenga siku rasmi ya kusikiliza na kutatua migogoro inayohusu ardhi katika Kata hiyo.
"Pamoja na kwamba kliniki hii itaendelea katika eneo hili la Nduli, wananchi wafahamu kwamba Ofisi zetu za ardhi zipo wazi, Ofisi ya kamishna, Ofisi ya ardhi Manispaa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, wakati wowote mnapokuwa na changamoto kuhusu masuala ya ardhi msisubiri kliniki au tusisubiri viongozi kuja huku sisi wenyewe twende ofisi hizo ili kutoa malalamiko au changamoto zilizopo, lakini pia ofisi za viongozi wote zipo wazi". Amesema Ngwada.
Mkuu wa Sekta ya Ardhi Manispaa ya Iringa, Ndg. Abenance Kamamonga amesema kuwa zoezi la kutatua migogoro ya wananchi kwa Kata ya Nduli linafanyika kwa siku 2 ambapo Siku ya kwanza itahusisha mitaa ya Mjimwema, Kilimahewa, Mapanda, Kipululu na Kisowele. Siku ya pili itahusisha Mitaa ya Mtalagala, Msisina na Njiapanda.
Akijibu swali la wananchi juu ya urasimishaji wa maeneo kwenye Kata hiyo, Kamomonga amesema kuwa wananchi ya Mitaa ya Kilimahewa, Mapanda na Mjimwema wameshaandika barua kwenye ofisi ya ardhi na tayari wameshalipia gharama za upimaji, hivyo zoezi hilo linatarajia kufanyika mapema wiki ijayo na kwamba huo ndio utakuwa mwarobaini wa malalamiko mengi ya Ardhi kwenye Kata hiyo.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa