WANANCHI wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wametakiwa kuwa chachu ya mabadiliko na kutambua kuwa wana jukumu la kujilinda wenyewe ili kupunguza kasi ya maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi(VVU) katika halmashauri hiyo.
Wito huo umetolewa na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Mhe. Ibrahim Ngwada,wakati wa maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo Disemba Mosi ya kila mwaka, ambapo kwa mwaka huu halmashauri hiyo imeadhimisha katika chuo kikuu cha Ruaha Catholic University(RUCU)kilichopo Manispaa ya Iringa.
Mhe.Ngwada amesema ni kweli maambukizi yapo kwa kiasi kikubwa katika halmashauri hivyo jukumu lao ni kujilinda.
"Sisi wenyewe tunapaswa kuwa chachu ya mabadiliko kwani jukumu kubwa ni kujilinda tu,"amesema Mhe.Ngwada.
Pia amesema,hali ya unyanyapaa katika halmashauri imepungua huku akitoa ushauri kwa vijana kutumia kinga ili kuepukana na ngono zembe ambazo zinaweza kuhatarisha afya zao.
Mmoja wa watu walioathirika na VVU Paulo Kiwela,amesema ameishi na virusi hivyo takribani miaka mitano huku akitumia dawa za kufubaza VVU.
Ambapo anaishi vizuri bila tatizo lolote hivyo alitumia fursa hiyo kuwashauri watu kujitokeza kupima bila kuamini imani za kishirikina ili pindi watakapo bainika kuwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi waanze kutumia ARVS.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Iringa Tinieli Mbaga,alitumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi juu ya kuzingatia masuala ya malezi chanya kwa watoto ili kuwatengenezea msingi mzuri huku akisisitiza juu ya kupinga ukatili wa kijinsia,kimwili na kingono.
Pia amewasihi wahanga wote wanaokutana na vitendo vya ukatili kuhakikisha wanapambana kikamilifu ili kuutokomeza kwa kushirikiana kikamilifu na Serikali.
Sanjari na hayo amesema kwa yeyote ambaye atashuhudia,kuhisi au kufanyiwa vitendo vya ukatili atoe taarifa katika vyombo husika vya serikali kama ofisi za ustawi wa jamii na dawati la jinsia ili kupunguza na kuweza kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa watoto na akina mama.
Aidha Mganga Mkuu Dr.Jesca Lebba.amegusia suala la chanjo dhidi ya UVIKO_ 19 kuwa inapatikana na haina madhara yeyote hivyo amewataka wananchi kuendelea kujitokeza kupata chanjo hiyo.
Katika maadhimisho hayo mbali na Msahiki Meya pia yalihudhuriwa na Naibu Meya mhe. Kenyata Likotiko na baadhi ya Madiwani wa Manispaa,wakuu wa Idara na vitengo.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa