Imeelezwa kuwa Shule mpya ya Sekondari ya Kwavava iliyopo Kata ya Kitwiru ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imetatua tatizo la wanafunzi waliokuwa wakitembea umbali mrefu wa takribani Kilomita 18 kwa miguu hapo awali kwenda Shule ya Sekondari ya Ipogolo kupata elimu kabla ya kuanzishwa kwa mradi wa shule hiyo.
Hayo yamebainika Januari O9, 2024 katika Ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge-TAMISEMI ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Dennis Londo ilipotembelea na kukagua mradi huo kwa lengo la kujionea maendeleo ya ujenzi pamoja na kufahamu changamoto zilizopo ili kuzitafutia utatuzi.
Awali akisoma taarifa mbele ya Kamati hiyo Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kwavava Mwl. Vick Kasanga amesema shule hiyo imekuwa ni suluhu kwa tatizo la muda mrefu kwa wanafunzi wa Kata hiyo kutembea umbali mrefu kufika shuleni jambo ambalo lilikuwa linadhoofisha ufanisi wa wanafunzi.
Aidha Mwenyekiti wa Kamati amepongeza jiitihada zilizofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Halima Dendego pamoja na timu nzima ya Menejimenti ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ikiongozwa na Mkurugenzi Ndg. Kastori Msigala kwa kukamilisha mradi huo kwa wakati huku ubora wa majengo yote ukiendana na thamani ya fedha zilizotolewa na kuacha maagizo ya kufanyika kwa maboresho madogo ya umaliziaji ujenzi ili kufanya muonekano wa majengo kuwa mzuri zaidi.
Mradi huo wa mpango wa kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP)
wenye thamani ya fedha za Tanzania shilingi 583,000,000/= ulianza kutekelezwa Agosti 2023 ambao una jumla ya majengo ya Madarasa 8, Ofisi 2 za Walimu, Jengo la Maktaba, Jengo la Tehama, Jengo la Utawala, Maabara 3, Vyoo vya Wasichana na Vyoo vya Wavulana.
Katika ziara hiyo ya siku moja Wajumbe wa Kamati ya Bunge- TAMISEMI walifurahishwa na jitihada za Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kuhamasisha wazazi na walezi kuwaleta wanafunzi shuleni kwani wameshuhudia muitikio mkubwa wa wanafunzi kufika shuleni na kuonya baadhi ya shule kudai michango lukuki kwa wazazi jambo ambalo limelikemewa vikali.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa