Kamati ya Fedha na Uongozi ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ikiongozwa na Diwani wa Kata ya Mkimbizi Mheshimiwa Eliud Mvela imefanya ziara ya kutembelea na kukagua baadhi ya Maduka yaliyopo Kata ya Mkwawa ndani ya Manispaa kwa lengo la kujiridhisha kwa wafanyabiashara kama wanatekeleza agizo la Serikari juu ya bei elekezi ya sukari.
Hatua hiyo imefikiwa mara baada ya baadhi ya wafanyabiashara kuuza bidhaa hiyo kwa bei holela ya Tsh. 4000/= hadi Tsh. 5000/= kwa kilo moja kitendo ambacho kimewafanya wananchi wengi kushindwa kumudu gharama hiyo.
Aidha Mhe. Mvela amesema kuwa katika ziara hiyo Kamati imebaini maduka mengi kutokuuza sukari kutokana na kuadimika kwa bidhaa hiyo na kwa maduka machache waliyokuta sukari ilikuwa inauzwa kwa bei elekezi ya Serikali ambayo ni TSh. 2800 hadi Tsh. 3200/= kwa kilo moja.
Mvela ametoa rai kwa wafanyabiashara kufuata bei elekezi na watakaokiuka agizo hilo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
“Nawaomba sana ndugu zangu wafanyabiashara muuze sukari kwa bei elekezi pia wale wanaoificha sukari waache tabia hiyo mara moja” Amesema Mvela
Kamati pia ilifanya ukaguzi wa leseni za biashara, Ushuru wa huduma, Ushuru wa taka ngumu na Kutoa elimu kwa wafanyabiashara kulipa kodi na tozo mbalimbali za Halmashauri kwa wakati.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa Mhe. Ibrahim Ngwada amesisitiza Wataalamu na Madiwani kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha mapato ya Halmashauri yanaongezeka.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Ndg. Kastori Msigala amesema amepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Kamati na kuhakikisha anayafanyia kazi kwa maslahi mapana ya Halmashauri na wananchi.
Ziara imehusisha Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Manispaa kwa kutembelea na kukagua miradi miwili ya Maendeleo ambayo ni Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Kitega Uchumi la Community Centre na mradi wa Ujenzi wa Jengo la Utawala Stendi mpya ya Igumbilo.
Jumla ya Kanda 5 zimetembelewa na Kamati ya Fedha na Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ambazo ni Kanda ya Mkwawa, Kanda ya Kihesa, Kanda ya Mlandege, Kanda ya Mkimbizi na Kanda ya Ruaha ambapo utaratibu huu utakuwa unafanywa na Kamati katika vikao vyake vya kila mwezi.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa