Na Mwandishi Wetu, Iringa
Kamati ya Uchumi, Afya na Elimu ya madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imewapongeza wataalam na kuwataka kutekeleza miradi yote inayotekelezwa katika Manispaa hiyo kwa ubora na kuikamilisha kwa wakati uliopangwa.
Kamati hiyo ilitoa pongezi na maagizo hayo kwa watalaam baada ya kufanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa katika Manispaa ya Iringa kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe.Eliud Mvela akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa kamati hiyo ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kutoa fedha za ujenzi huo pamoja na Halmashauri kwa mchango na ushirikiano wao katika kuendeleza ujenzi wa Kituo cha Afya Mkimbizi.
Mhe.Mvela ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mkimbizi, alisema ujenzi wa kituo hicho utakapokamilika utapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto za wananchi kupata huduma za matibabu.
"Tunamshukuru mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wote kwa kutuona watu wa Mkimbiziā alisema Bi. Fatuma Sultan Mkazi wa eneo hilo.
Mbali na kituo cha afya Mkimbizi, madiwani wa kamati hiyo walitembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa choo cha shule ya msingi Ukombozi, ujenzi wa maabara shule ya Sekondari Miyomboni, madarasa ya shule ya Sekondari Mivinjeni.
Miradi mingine waliyokagua ni ujenzi wa machinjio ya kisasa Ngelewala, vibanda vya biashara Mlandege, choo cha shule ya msingi Igumbilo na ujenzi wa choo cha stendi ya Igumbilo
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Ndg. Omary Mkangama ameishukuru kamati hiyo kwa ukaguzi wa miradi na ameahidi kuyafanyia kazi maagizo yote ambayo kamati imeyatoa.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa