Mkuu wa Mkoa wa Iringa mhe.Queen Sendiga ameagiza ifikapo Agosti mwaka huu, ujenzi wa bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Ipogolo uwe umekamilika.
Mhe.Sendiga ametoa maagizo hayo June 8 alipokuwa katika ziara ya kikazi ya ukaguzi wa miradi mbali mbali inayotekelezwa na Halmashauri ya Manispaa kwa kutumia fedha kutoka Serikali kuu na mapato ya ndani.
Aidha mhe Sendiga amemtaka Mkurugenzi kuweka mikakati madhubuti ambayo itafanikisha ukamilishaji wa bweni hilo kwani likikamilika litaondoa adha ya wanafunzi hao inayowakabili hivi sasa.
'Serikali imetoa fedha ili kujenga bweni kwa lengo la kuwafanya wanafunzi hawa wenye mahitaji maalum waweze kusoma bila changamoto zozote,ipo haja Manispaa kukamilisha miradi hii inayosuasua kwa wakati ili itumike na wananchi kama mhe.Rais Samia SuluhuHassan alivyokusudia alisema Sendiga.
Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi ndugu Charles Mwakalila amesema kwa mwaka wa fedha 2021/2022 wametenga bajeti ya sh.milioni 30 ambazo pamoja na mambo mengine pesa hizo zitatumika katika ukamilishaji wa bweni hilo pamoja na uzio kwa ajili ya usalama shuleni hapo.
Katika ziara hiyo miradi mingine iliyokaguliwa ni Ujenzi wa Shule ya Sekondari ya IIsakalilo,ujenzi wa kituo cha afya Itamba na Ujenzi wa Machinjio ya kisasa ya Ngelewala
Dr.Stephen Ngwale ni Afisa Mifugo wa Manispaa anasema shughuli zinazofanyika kwa sasa katika Machinjio ya Kisasa ya Ngelewala ni ujenzi wa kisima,kuweka mfumo wa maji moto na maji baridi,kujenga mabwawa ya maji machafu na mifereji yake .
Pia Dr Ngwale anabainisha kuwa mradi huo ukikamilika wanatarajia kuchinja ng,ombe mia moja (100),Mbuzi mia mbili(200) kwa siku na kuwa manufaa ya mradi huo pindi utakapoanza kufanya kazi utatoa ajira zisizo rasmi kwa zaidi ya vijana 200, kuongeza mapato ya Halmashauri na kuimarisha usafi wa mazingira kwa kudhibiti uchinjaji holela.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Mhe.Ibrahim Ngwada amesema ziara ya Mkuu wa Mkoa imewafumbua macho na kuwa kama kiongozi mkuu wa Halmashauri atahakikisha miradi inakamilika na ikiwa na ubora unaohitajika kulingana na thamani ya fedha zilizopangwa.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa