Katibu mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa Mhandisi Joseph Nyamhanga amekabidhi jumla ya Tshs Milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa uzio kwenye shule ya wasichana ya Iringa.
Mhandisi Nyamhanga ametoa kiasi hicho katika ziara ya siku moja aliyoifanya katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kwa ajili ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.
Akipokea fedha hizo mkuu wa shule ya sekondari ya wasichana Iringa Bi Blandina Daniel ameshukuru kwa msaada huo na kumpongeza Rais wa jamhuri wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kwa kuwathamini wanafunzi na walimu wa shule kwa kutoa zaidi ya shs milioni mia saba ili kuboresha majengo yaliyopo shuleni hapo.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Bi.Hapiness Seneda amewataka wanafunzi kusoma kwa bidii na kupunguza daraja la sifuri kwani Serikali imejitahidi kwa kiwango kikubwa kutatua changamoto zilizokuwa zinawakabili hapo awali.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya ukarabati wa shule hiyo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Bw Hamid Njovu amesema kuwa anampongeza mkuu wa shule hiyo kwa usimamizi mzuri wa mradi huo na kuwa Halmashauri imechangia kiasi cha shilingi Millioni kumi na moja (11,000,000) ili kumalizia ujenzi wa uzio wa shule unaoendelea kujengwa shuleni hapo.
Ziara hiyo ya siku moja ilifanyika kwa kutembelea miradi ya Machinjio ya Manispaa iliyopo kata ya Mwangata eneo la Ngelewala ambapo Katibu Mkuu alipata fursa ya kujionea changamoto zilizopo na kuahidi kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.
Katika ziara hiyo Mhandisi Nyamhanga pia alitembelea na kukagua Hospitali ya wilaya ya Frelimo ambapo Mganga Mkuu Manispaa Dr. Jesca Lebba alitaja changamoto zilizopo kuwa ni ukosefu wa majengo ya wodi ya wanaume,wanawake watoto na ukosefu wa wodi ya wagonjwa mahututi pamoja na chumba cha kuhifadhia maiti.
Ziara hiyo imeshirikisha viongozi mbalimbali wa Serikali, wataalamu kutoka wilayani, Mkoani na Manispaa ya Iringa akiwepo Katibu tawala wa Mkoa.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa