Rai imetolewa kwa jamii kuhamasisha kinamama wajawazito kuhudhururia Kliniki mapema pindi wanapohisi wana ujauzito ili kupatiwa nyongeza ya vitamin na madini ambazo humkinga mtoto kuzaliwa na matatizo mbalimbali ya kiafya.
Akitoa rai hiyo Afisa lishe wa Manispaa ya Iringa Bi.Anzaeli Msigwa ametaja madhara wanayoweza kupata wajawazito kwa kuchelewa kuanza Kliniki ni pamoja na kuzaa watoto wenye matatizo ya mgongo wazi, mdomo Sungura na kuzaa watoto wenye vichwa vikubwa hivyo hurudisha nyuma uchumi wa familia kwa ajili ya kutafuta matibabu ya magonjwa hayo
Anzael ameitaka jamii kuzingatia lishe bora pamoja na kuzalisha vyakula vyenye virutubishi kwa wingi kama viazi lishe, maboga lishe n.k
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa Omary Mkangama amewataka watendaji wa Kata na Mitaa pamoja na Maafisa Ugani wote kushirikiana kwa bidii na wahudumu wa afya ya msingi waliopo katika kila mtaa kutekeleza viashiria vya mkataba kwa weledi kwa kupima hali ya lishe ya watoto chini ya miaka mitano, kuwaibua watoto wenye utapiamlo ili waweze kupatiwa tiba, kufanya maadhimisho ya siku ya afya na lishe pamoja na kutembelea kaya zenye wajawazito na watoto chini ya miaka mitano na kutoa elimu ya lishe
Mstahiki Meya Manispaa ya Iringa Mhe. Ibrahimu Ngwada amewataka Madiwani na Watendaji kushirikiana kuhamasisha jamii iweze kulima bustani za mbogamboga na matunda katika maeneo yao hasa mashuleni ili kusaidia jamii kupata lishe bora na kuimarisha afya zao.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Ndugu Richard Kasesela ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kikao hicho amewapongeza Watendaji wote kwa jitihada wanazofanya kuhakikisha viashiria vya Mkataba vinatekelezwa ipasavyo ili kuondoa matatizo ya lishe katika Manispaa yetu.
Kikao hicho cha tathmini ya Mikataba ya lishe kimefanyika tarehe 28/1/2021 katika ukumbi wa Chuo kikuu Huria na walengwa walikuwa ni Waheshimiwa Madiwani, Watendaji wa Kata ,Maafisa Maendeleo wa kata, Wajumbe wa kamati ya lishe, Muwakilishi wa Wahudumu wa afya ngazi ya jamii na Wadau wa lishe ambao ni ASAS, TAHEA, ALAMANO, LISHE ENDELEVU, PAPA YOHANE, CALLAFRICA, USAID-NAFAKA NA USAID-MBOGA NA MATUNDA
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa