Kamati ya kudhibiti Ukimwi katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ikiongozwa na Mwenyekiti Kenyatta Likotiko ambaye pia ni Naibu Meya imefanya ziara ya kutembelea kikundi cha ITIKA kilichopo kata ya Mwangata, na zahanati ya Itamba.
Ziara hiyo imefanyika leo tarehe 22/10/2021 kwa lengo la kuona maendeleo na kusikiliza changamoto na kuzitafutia ufumbuzi
Awali akisoma taarifa juu ya uendeshaji wa kikundi hicho kinachojishughulisha na uokaji wa mikate,katibu wa kikundi Bi.Haika Luisa amesema kikundi kina jumla ya wanachama kumi na sita,wanawake kumi na nne na wanaume wawili, ambao waliweza kupatiwa mafunzo juu ya utengenezaji wa mikate.
Alisema pia, kikundi kilipata msaada wa mashine ya kisasa ya kuoka mikate kutoka shirika la lisilo la Kiserikali Allamano yenye thamani ya shilingi milioni Arobaini ( 40,000,000)
Pia walipata mkopo kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kiasi cha shilingi milioni tano, na shilingi milioni Moja ikiwa ni ruzuku kwa vikundi vyenye mahitaji maalum kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa, kwa lengo la kufanikisha shughuli za kikundi.
Haika alisema kikundi kinaweza kutumia kuanzia kilo 75 za unga wa ngano kwa siku na kuzalisha mikate hadi kufikia mia tatu hamsini kwa siku, ambayo ikiuzwa hupatikana wastani wa shilingi 247,000. Mikate hii huuzwa kwa wakazi wa maeneo ya jirani na maeneo ya mjini ikiwemo kwenye Taasisi mbalimbali za jirani.
Kikundi kimefanikiwa kununua trei 111 kwaajili ya kuokea mikate zenye ukubwa tofauti tofauti zenye thamani ya 780,000.
Alisema changamoto walizonazo ni ukosefu wa usafiri kwaajili ya kusambaza mikate katika maeneo ya mbali kama vile Kata ya Ruaha, Igumbilo na Kitwiru, Upungufu wa trei 89 kwa ajili ya kuoka mikate, pia upungufu wa mitungi ya gesi.
Kamati iliweza kutembelea pia zahanati ya Itamba kwa lengo la kufuatilia utoaji wa huduma katika kliniki ya VVU ya tiba na mafunzo kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa mbele ya kamati hiyo juu ya uendeshaji washughuli za kituo hicho ilionyesha kuwa kituo kimefanikiwa kutoa huduma ya utoaji dawa za kufubaza virusi vya ukimwi pamoja na Kifua kikuu. ushauri na mafunzo mbalimbali.
Hata hivyo, Zahanati ya Itamba imebainisha ukosefu wa mshine ya kupimia CD4 pamoja na chumba cha uangalizi na matibabu kwa watu wanaochukua dawa za kufubaza virusi vya ukimwi kwani kilichopo ni kidogo na hakina usiri.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa