KITUO cha Afya cha Mkimbizi kilichopo kata ya Mkimbizi katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kinachojengwa kwa gharama ya Shilingi milioni 250 ambazo ni fedha za tozo ya miamala ya simu kinatarajia kutoa huduma kwa wananchi zaidi ya 15,000.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Iringa, Dk.Jesca Lebba alisema hayo baada ya timu ya menejimenti ya manispaa hiyo ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Iringa, Gerald Mwamuhamila ilipotembea kukagua ujenzi wa mradi huo Februari 3, 2022 ambapo ilifurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi huo.
Dk.Lebba alisema ujenzi wa kituo hicho utakapokamilika mara baada ya kukamilika utahudumia wananchi zaidi ya elfu 15 wa kata ya Mkimbizi na kata jirani za Mtwivila na Kihesa.
Alisema hadi sasa majengo matatu ambayo ni jengo la wagonjwa wa nje, vyoo vya mashimo 10 pamoja na maabara vimekamilika ambapo hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu mradi wote unatarajia kukamilika.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Kata ya Mkimbizi, Adam Kondo, aliishukuru Serikali pamoja na Menejimenti ya Manispaa kwa kuleta mradi huo ambao unakwenda kupunguza adha ya huduma za Afya katika eneo lake.
Naye Yoel Mashimba mkazi wa Mkimbizi alishukuru kwa ujenzi wa mradi huo kwenye kata yao ambapo utakapo kamilika utawasaidia wananchi kuacha kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Aidha, miradi mingine iliyotembelewa na menejimenti ya Manispaa ya Iringa ni pamoja na Shule ya Msingi JJ Mungai, Hospitali ya Flerimo, Shule ya Msingi Ulonge, Stendi ya mabasi Igumbilo, pamoja na Shule ya Msingi Nyumbatatu.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa