Mkuu wa Wilaya ya Iringa Komredi Kheri James ametaka kutekelezwa kwa maagizo aliyotoa kwa wamiliki na madereva daladala na sio kutoa ahadi ili kutatua changamoto zilizopo na kustawisha huduma ya usafiri ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.
Komred Kheri amesema hayo wakati akifungua kikao cha kusikiliza kero na changamoto za wamiliki na madereva Daladala kilichofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo.
“Nataka kuona maagizo ninayotoa katika kikao hiki utekelezaji wake unaanza mara moja kwenye kikao hiki sihitaji ahadi bali nahitaji utekelezaji kuanza mara moja.” Amesema Komred Kheri
Hatua hii imefikiwa mara baada ya Madereva na Wamiliki wa Daladala kufanya mgomo wa takribani siku 3 mfulizo bila kutoa huduma za usafiri kuanzia tarehe 6-8/5/2024 na kusababisha adha kwa abiria, kwa madai mbalimbali ikiwemo kuvunjwa kwa makubaliano baina ya Daladala na Umoja wa Madereva Bajaji yaliyosainiwa mbele ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa Mhe. Halima Dendego na Mstahiki Meya Mhe. Ibrahim Ngwada tarehe 13 Julai 2023 katika Uwanja wa Mwembetogwa.
“Mwanasheria na Afisa Biashara mnazo sheria ndogo za Halmashauri ambazo mnapaswa kuzisimamia Mgambo mnao na OCD atakuwa nanyi katika usimamizi wa utekelezaji wa sheria hizo, hivyo jipangeni kufanya kazi hiyo kuanzia tarehe 15.05.2024 kukamata wale wote watakaokiuka taratibu muweze kuwachukulia hatua za kisheria na kila wiki mnatakiwa kunipa taarifa na changamoto mtakazokabiliana nazo wakati wa utekelezaji ili nizishughulikie.” Amesema Komredi Kheri
Mfawidhi LATRA Mkoa wa Iringa Ndg. Joseph Umoti amesema kuwa wamebaini asilimia 90 ya madereva bajaji hawana sifa pia baadhi ya madereva huacha masomo na kukimbilia kuendesha bajaji hivyo ameonya kuacha tabia hiyo mara moja kwani mamlaka itahakikisha sheria, kanuni na taratibu zinafuatwa.
Mwenyekiti wa Umoja wa Daladala Ndg. Rashid Mshana amesema kukosekana kwa usimamizi toka kwa mamlaka zinazohusika ndio imepelekea madereva Bajaji kuvunja sheria na kukiuka makubaliano ya njia waliyopangiwa na kupelekea wao kufanya mgomo.
Katibu wa Umoja wa Daladala Manispaa Ndg. Shaibu Maluzuku amesema uwepo wa vituo binafsi vidogo vya mabasi (Terminal) vilivyopo katikati ya Mji vimekuwa ni kiwazo kwao kwani vinasababisha wao kukosa abiria.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa