MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE MANISPAA YA IRINGA YAFANA.
WANAWAKE WAJITOKEZA KWA WINGI
Wanawake wa Manispaa ya Iringa wameungana na wanawake wote Duniani kuadhimisha kilele cha siku ya wanawake ambayo hufanyika tarehe 8/3 kila mwaka.
Katika Maadhimisho hayo yaliyopambwa na maandamano yaliyoanzia ofisi za Manispaa ya Iringa kuelekea viwanja vya Mwenbetogwa ambako ndio maadhimisho yalihitimishwa nderemo,vifijo,shangwe na vigelegele vilisikika toka kwa wanawake walioshiriki huku wakiimba nyimbo kwa furaha.
Mgeni rasmi Mbunge wa Jimbo la Iringa mjini Mhe.Jesca Msambatavangu amesema kina mama wanaaminika katika jamii kwa kufanya mambo kwa weledi kama kauli mbiu inavyosema wanawake katika Uongozi,Chachu kufikia Dunia yenye usawa.
Mhe.Msambatavangu amewataka wanawake kugombea nafasi za uongozi na kuonyesha uwezo pale wanapopata nafasi kwa kuwa wao ni viwanda hivyo wanatakiwa kutoa bidhaa bora.
Kabla ya kilele cha maadhimisho hayo Wanawake walipata fursa ya kujengewa uwezo katika masuala mbali mbali kama Ujasiriamali,Mirathi, Sheria ya Ndoa pamoja na wanawake na uongozi.
Mstahiki Meya wa Manispaa mhe.Ibrahim Ngwada amesema anawapongeza wanawake kwa siku hii muhimu kwao na anathamini na kuwaunga mkono wanawake katika jitihada mbali mbali wanazozifanya katika kujikomboa kiuchumi.
Mhe Ngwada amechangia fedha kiasi cha shilingi laki tano kwa ajili ya kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Sherehe hizo zilihitimishwa kwa mgeni rasmi kupokea zawadi kutoka kwa wakina mama wa vikundi mbali mbali,Taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali ambao wamejitoa kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Zawadi hizo ni pamoja na Sabuni,Madaftari,Mchele unga, Sukari, mafuta ya kupikia na fedha kama ishara ya upendo kwa watoto hao.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa