MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amefunga mafunzo ya wakufunzi wa sensa wa ngazi ya Taifa leo mjini Iringa huku akitoa taarifa kwamba maandalizi yake yamekwishafika asilimia 87.
Mafunzo hayo yaliyoshirikisha wakufunzi zaidi ya 400 yamefanyika kwa siku 21 katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa, mjini Iringa, yakihusisha watakwimu na wachumi.
Akifunga mafunzo hayo, Abdulla ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Taifa ya Sensa alisema sensa hiyo itakayofanyika Agosti 23 mwaka huu itakuwa ya aina yake kwani itatumia mfumo wa kidigitali na itaunganisha mazoezi makubwa mawili.
“Sensa hii itaunganisha mazoezi mawili muhimu ambayo ni sensa ya majengo na sensa ya anwani za makazi,” alisema na kuwataka watanzania kutoa ushirikiano kwa makarani kwa kutoa taarifa sahihi na za kweli.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa alisema; “Baada ya wakufunzi hawa wa kitaifa kumaliza mafunzo yao, hatua inayofuata ni kwenda kuwafundisha wakufunzi wa ngazi ya mikoa ambao nao, watawafundisha wakufunzi wa ngazi za wilaya.”
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Hassan Chande aliwataka wote waliopewa kazi hiyo wakaifanye kwa uaminifu na kuwahakikishia kwamba wizara yao haitakuwa na kigugumizi kutoa fedha zinazohitajika kufanikisha zoezi hilo.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene alisema pamoja na maandalizi ya sensa hiyo kufikia asilimia 87, utengaji wa maeneo ya kijiografia kwa ajili ya kuhesabia watu umekamilika kwa asilimia 100.
“Pamoja na mafanikio hayo makubwa bado kuna uhitaji mkubwa wa uhamasishaji na uelimishaji wa sensa ili kila mwananchi aone umuhimu wa kuhesabiwa na kutoa taarifa zote atakazoulizwa,” Simbachawene alisema.
Wengine waliokuwepo katika hafla hiyo ni pamoja na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete aliyesema sensa hiyo itaisaidia wizara yake kupanga matumizi bora ya ardhi.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa