"naagiza kesho kila aina ya basi ipatiwe chumba cha kukatisha tiketi katika stendi mpya ya Igumbilo na wakalipie, endapo kama watakaidi basi naamini hili lipo ndani ya kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hivyo watashughulika nao"
Hayo yamesemwa Septemba 22, 2022 na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Mhe. Ibrahim Ngwada katika kikao cha Baraza Maalum la Madiwani la kupitia taarifa ya mwaka 2021/2022 lililofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Manispaa.
Aidha Mstahiki Meya amesema kama watakaidi itakuwa ni kurudishana nyuma kimaendeleo ambayo yamefanyika katika ujenzi wa Stendi hiyo mpya ya Mabasi ya Mikoani Igumbilo kwa kupoteza mapato.
Sambamba na hayo akamuagiza Mkurugenzi na Mhandisi majengo kwenda mara moja katika Stendi hiyo na kuvunja vibanda vyote visivyo rasmi ambavyo vinatumika kukatisha tiketi na jengo la utawala lianze kufanya kazi mara moja
Awali akiwasilisha hoja hiyo mbele ya wajumbe wa Baraza Mhe. Boniface Kilave, Diwani wa kata ya Igumbilo amesema Manispaa imekuwa inapoteza mapato kutokana na hali ya wamiliki wa mabasi kutumia vituo ambavyo sio rasmi kukatisha tiketi jambo ambalo sio sahihi akitolea mfano matumizi ya eneo la pembezoni mwa barabara karibu na Stendi ya zamani ya Ipogolo
Aidha Mhe. Meya Ibrahim Ngwada amewataka wataalam wa Manispaa kusimamia vyema ujenzi wa Miradi ya Maendeleo katika kila Kata na kuhakikisha wananchi wananufaika nayo vilivyo
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe.Mohamed Moyo ameonya tabia baadhi ya wajumbe wa timu ya Menejimenti kutokufanyia kazi maazimio yanayotolewa katika vikao mbalimbali na kumtaka Mstahiki Meya kutolifumbia macho suala hilo kwani linadhoofisha maendeleo ya Manispaa .
*Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Manispaa ya Iringa*
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa