Hatimaye Machinjio ya kisasa ya Ngelewala iliyopo Manispaa ya Iringa imeanza kazi Rasmi leo 12/7/2022 ambapo mpaka sasa jumla ya Ng'ombe sabini na moja (71) Mbuzi saba (7 )na kondoo mmoja (1)wamechinjwa katika machinjio hiyo mpya.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe.Mohamed Moyo amesema kwa zaidi ya miaka kumi(10) kumekuwa na kusuasua kwa ujenzi wa mradi huo kupelekea uongozi wa ngazi ya Wilaya na Mkoa kuamua kuusimamia kwa karibu ili machinjio hiyo ikamilike na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa Manispaa ya Iringa
Dr.Steven Ngwale ni Mkuu wa Idara ya mifugo na Uvuvi Manispaa amesema Machinjo hiyo ilianza kujengwa mwaka 2008 na imegharimu jumla ya shilingi bilioni mbili na kuwa inauwezo wa kuchinja ng'ombe mia moja(100), Mbuzi mia mbili(200) kwa siku.
Aidha Dr.Ngwale amesema manufaa ya mradi huo ni kutoa ajira kwa vijana zaidi ya 200,kuongeza mapato ya Manispaa na utunzaji wa mazingira.
Pia Dr.Ngwale ametoa wito kwa wachinjaji wote kuwa, kuanzia tarehe 12/7/2022 wafanyie shughuli za uchinjaji katika Machinjio hiyo mpya ya Ngelewala na si vinginevyo.
Naye Bw.Robert Lugenge ni mmoja wa wachinjaji waliopo katika Machinjio ya Ngelewala anasema wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo za kuwajengea Machinjio hiyo nzuri kwani kwa sasa machinjio hiyo wanayoitumia ina ubora unaotakiwa hivyo kurahisisha shughuli zao za uchinjaji tofauti na machinjio za awali ambazo zilikuwa zimechakaa.
Mkuu wa wilaya ya Momba Mhe.Faki Lulandala aliyeambatana na Mkuu wa Wilaya ya Iringa amewapongeza viongozi na wataalamu kwa juhudi kubwa walizofanya kukamilisha mradi huo mkubwa na kuahidi kutembelea tena huku akiambatana na waheshimiwa Madiwani wake wa wilaya ya Momba Mkoani Songwe kwa lengo la kujifunza zaidi.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa