Na Mwandishi Wetu,Iringa
HALMASHAURI ya Manispaa ya Iringa Mkoani hapa imeshika nafasi ya pili kitaifa katika mashindano ya usafi wa mazingira kwa mwaka 2021.
Hayo yameelezwa leo (Januari 26) na Kaimu Mkuu wa Idara ya Usafi na Mazingira wa Manispaa ya Iringa, Mohamed Mtopa kwenye mkutano wa Baraza la Madiwani la kupokea taarifa kutoka kwenye Kata kwa kipindi cha Robo ya Pili (Octoba – Disemba, 2021/2022 uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Manispaa hiyo.
Mtopa alisema kata za Gangilonga, Ruaha, Kitanzini na Miyomboni zimefanya vizuri zaidi katika mashindano hayo ya usafi na hivyo kuifanya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kushika nafasi ya pili kitaifa.
Aidha, Mtopa aliitaja mitaa ya Kilimani, lugalo A, kinyanambo C, Jamati, Maweni, Miyomboni, Mlambalazi, Mapinduzi, Ngen’gena na Makondeko iliyopo ndani ya kata hizo kuwa imefanya vizuri sana katika usafi wa Mazingira.
Kufuatia Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kufanya vizuri katika usafi kitaifa, Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Mhe. Ibrahim Ngwada, aliahidi kikao kijacho kuzikabidhi hati za pongezi kata zilizofanya vizuri katika usafi.
Mhe. Ngwada amesema kufanyika kwa tukio hilo ni hamasa kwa waliofanya vizuri lakini pia kwa wengine kuongeza jitihada ili msimu ujao na wao wapate zawadi hiyo kwa kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi katika utunzaji wa mazingira.
Aidha, Mhe. Ngwada amewapongeza Madiwani, Watendaji na Wataalamu wa Manispaa kwa ushindi huo na kuwataka waendelee kuyatunza mazingira ili yawe masafi muda wote na msimu ujao washike nafasi ya kwanza kitaifa.
Mwisho
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa