"Ndugu waandishi wa habari hili jambo na uvumi kuhusu Manispaa ya Iringa ina uhaba wa kondomu sio kweli, ukweli ni kwamba Manispaa yetu inazo kondomu za kutosha katika maeneo yote ya muhimu kuwepo"
Hayo yamesemwa leo tarehe 2/9/2021 na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Mhe. Ibrahim Ngwada katika kikao chake na waandishi wa Habari kilichofanyika katika ofisi yake kwa lengo la kutoa ufafanuzi kutokana na baadhi ya vyombo vya habari kuripoti taarifa iliyosema Madiwani Manispaa ya Iringa walalamikia upungufu wa kondomu
Aidha Mhe. Ngwada amesema taarifa hiyo sio nzuri na haina ukweli wowote kwani Serikali yetu ina wajali wananchi wake na imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha inapambana kupunguza maambukizi ya Ukimwi Mkoani Iringa hususani Manispaa
Vilevile amesema, chanzo cha hoja hiyo iliibuliwa katika Mkutano wa Baraza la Madiwani lililofanyika siku ya tarehe 31.08.2021 ambapo Mhe. Tandes Sanga Diwani wa Kata ya Ruaha kusema alipita katika baadhi ya nyumba za kulala wageni na kukosa kondomu katika maeneo hayo
Katika maelezo yake Mhe. Ngwada amesema jambo hilo linawezekana kwakuwa kondomu zikiwekwa zinatumika mara moja hivyo zinapoisha wataalamu husambaza tena na kusema inaonyesha muitikio wa wananchi kutumia kondomu ni mkubwa, hivyo amesema isichukuliwe tafsiri ya kwamba kuna upungufu wa kondomu ndani ya Mansipaa yake
"Katika kipindi cha miezi miwili tumegawa jumla ya kondomu laki moja, sitini na nane elfu na mia tano (168, 500) katika maeneo mbalimbali ya taasisi za kiserikali na binafsi hivyo huwezi kusema kondomu hakuna na kumbuka zoezi hili ni la mara kwa mara" Ngwada alisema
Naye Bi. Dora Myinga ambaye ni Mratibu wa kudhibiti Ukimwi Sekta ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Iringa amesema, utofauti wa idadi ya ugawaji wa kondomu katika maeneo, unatokana na uwepo wa viashiria na vichocheo vingi vya maambukizi ya virusi vya ukimwi kama vilabu, vyuo na sehemu za starehe, nyumba za kulala wageni kwa kuwa na matukio ya kingono mengi hali ambayo inawalazimu kugawa kwa wingi kinga hizo katika maeneo hayo
Akihitimisha kikao hicho Mhe. Ngwada ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi huku akibainisha kuwa Mkoa wa Iringa ni wa pili kwa maambukizi ya VVU/UKIMWI.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa