Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa mhe.Ibrahim Ngwada ameyataja mafanikio na ubora wa miradi mbalimbali iliyotekelezwa ndani ya Manispaa ya Iringa kwa mwaka wa fedha 2021/2022 huku akizipongeza kamati za kudumu za Halmashauri kwa usimamizi mzuri wa miradi hiyo ya maendeleo.
Hayo ameyasema leo Agasti 17/2022 katika Mkutano wa Baraza la Madiwani wa kuwasiliana na kujadili taarifa za robo ya nne ya mwaka 2021/2022, lililofanyikab katika ukumbi wa Mikutano wa Manispaa ya Iringa
Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho ameyataja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na ukamilishaji ujenzi wa Machinjio kubwa ya Ngelewala yenye uwezo wa kuchinja ng'ombe 100 na mbuzi 200 kwa siku, ukamilishaji wa wodi ya kina baba na kina mama, jengo la upasuaji pamoja na chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospital ya Wilaya ya Iringa (Frelimo)
Miradi mingine ni ujenzi wa Shule na Madarasa, zahanati, vituo vya afya, Masoko, Stendi ya mabasi pamoja na usimamizi mzuri wa usafi wa mazingira.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini Mhe. Jesca Msambatavangu ambaye ni mjumbe katika Baraza hilo amesema anatamani kwa mwaka mpya wa fedha 2022/2023 vipaumbele viwe katika ujenzi wa shule za msingi katika kukarabati na ujenzi wa madarasa hasa shule zilizopo pembezoni mwa Halmashauri.
"Kutokana na hali ya uchakavu na changamoto shule zetu nyingi za msingi, tunaomba Halmashauri ifanye kipaumbele kwa awamu hii ili kuona watoto wetu wanapata Elimu kwa urahisi ili kutimiza ndoto zao" Mhe Jesca alisema
Hata hvyo Mhe. Mohamed Moyo, Mkuu wa Wilaya ya Iringa amempongeza Mkurugenzi kwa jitihada walizofanya kukusanya mapato hadi kuvuka lengo
Pia Mhe. Moyo amekemea jambo la ukatili wa kijinsia kuendelea kushamiri katika baadhi ya maeneo ya Manispaa ya Iringa na kuwataka Madiwani kuendelea kulikemea suala hilo katika maeneo yao na kuchukua sheria stahiki kwa wale wote watakaoshiriki ama kubainika wamefanya ukatili wa kijinsia.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa Ndg. Gerald Mwamuhamila amewataka wananchi wote ambao maeneo yao yalichukuliwa na Halamashauri huku wakidai fidia kuwa wawe wavumilivu kwani ameshamuagiza Mkuu wa Idara ya Mipango Miji kushughulikia suala lao la kulipwa fidia zao
Akihitimisha kwa kufunga Baraza hilo Mstahiki Meya Mhe. Ibrahim Ngwada amempongeza mwenyekiti wa kamati ya maadili Mhe. Mahazi Epautwa, Diwani wa Kata ya Kitanzini kwa kufanikiwa kusimamia vizuri kamati yake ya Maadili kwa kipindi cha Robo zote kwa mwaka huu.
Mwisho amewataka Madiwani kuendelea kuzungumzia mazuri yanayoendelea kufanyika ndani ya Halmashauri chini ya Uongozi wa Rais wa Awamu ya sita ya Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa