MANISPAA YA IRINGA INATARAJIA KUKUSANYA BILIONI 8 KWA MWAKA WA FEDHA 2024/2025.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Mhe. Ibrahim Ngwada amesema kuwa Manispaa ya Iringa inatarajia kukusanya fedha kiasi cha shilingi Bilioni 8 kwa mwaka wa fedha 2024/25 kutokana na mapato kuongezeka na kufikia shilingi Bilioni 6.7 kwa mwaka wa fedha uliopita.
Hayo ameyasema katika Mkutano wa Mwaka wa Baraza la Madiwani kwa kipindi cha Mwaka wa Fedha 2023/24, ambao umefanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Iringa Tarehe 09 Septemba, 2024 kwa lengo la kujadili taarifa ya utendaji kazi na uwajibikaji katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, na kufanya uchaguzi wa Naibu Meya na Uteuzi wa wajumbe wa
kamati za kudumu za Halmashauri
"Moja ya mafanikio makubwa katika Halmashauri ambayo tunajivunia ni kupandisha mapato yetu kutoka shilingi Bilioni 3.5 kwa miaka iliyopita mpaka kufikia shilingi Bilioni 6.3 kwa mwaka wa fedha 2023/24 ambapo makisio ilikuwa ni Bilioni 6.7. Hakika tumepanda kwa kiwango kikubwa. Kutokana na hilo tunaweza kukusanya kiasi cha Bilioni 8 kwa Mwaka wa fedha 2024/25". Amesema Ngwada.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Komredi Kheri James ameupongeza uongozi wa Halmashauri kwa uwajibikaji uliotukuka katika kuwahudumia wananchi kwa mwaka wa fedha uliopita,pia ametoa msisitizo kwa uongozi huo kuwa mwaka unapokamilika inatakiwa wajipange hasa katika masuala ya ukusanyaji wa mapato, usimamizi wa
miradi, usikilizaji na utatuzi wa kero za wananchi, usafi pamoja na kuboresha maamuzi na kusimamia biashara na huduma bora ndani ya Manispaa.
"Uwepo wa Halmashauri zetu za wilaya au Manispaa ni dhamira ya kuwasogezea wananchi bunge lao la kujadili mambo yao, yanayostawisha dhamira zao Kupitia Baraza hili tumeshuhudia mipango mikubwa ya maendeleo liyopangwa inatekelezwa, pamoja na maamuzi yaliyopangwa kwa faida ya wananchi na tumeshuhudia maono makubwa yaliyopo kwa ajili ya leo na kesho, nina imani mtahakikisha maamuzi yenu yanagusa maisha ya watu". Amesema Kheri.
Naye Katibu wa CCM wilaya ya Iringa Mjini Ndg, Hassan Makoba ametoa rai kwa Madiwani kuwa mabalozi wazuri kwa wananchi katika Kata zao kwa kuwaeleza
mambo makubwa ambayo yamefanywa na Baraza la Madiwani kiujumla kwa maslahi ya Kata zao,pia ameshauri mambo yote yanayopangwa na Madiwani wayasimamie maana wao ndio wenye dhamana kubwa ya kusimamia Manispaa ya Iringa na kuwa wanapotekeleza hayo wanatekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mkutano huo umehudhuriwa na Kamati ya Siasa ya Wilaya, Mkuu Wa Willaya, Katibu Tawala wilaya, Madiwani, Sekretariati ya Mkoa, wawakilishi wa Taasisi mbalimbali za Serikali kama TARURA, IRUWASA, TAKUKURU, TANESCO, TANROAD, Wakuu wa Idara na Vitengo wa Manispaa, watendaji wa Kata, watumishi pamoja na wananchi.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa