Na Mwandishi Wetu, Iringa
MSTAHIKI Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Mhe.Ibrahimu Ngwada, ameitaka jamii kupinga na kukemea kwa nguvu zote vitendo vya ukatili wa watoto na wanawake ambavyo vinaonekana kukithiri.
Alisema kesi za ukatili dhidi ya watoto na wanawake ni nyingi hivyo tunapaswa kupinga ukatili huu kwa nguvu zote na kukemea matendo hayo yasiyokuwa na maadili.
Alisema hayo wakati maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto ambapo Halmashauri ya Manispaa ya Iringa iliazimisha siku hiyo kwa kufanya maandamano yaliyoongozwa Mhe.Ngwada.
Kilele cha maadhimisho hayo hufanyika Disemba 10 kila mwaka Duniani kote na kwa mwaka 2021 Manispaa imeadhimisha kwa kufanya maandamano yaliyoanzia eneo la FFU Kata ya Kihesa na kumalizia kwenye uwanja wa Shule ya msingi Mlandege.
Akizungumza baada ya maandamano hayo, Mhe. Ngwada alisema inakatisha tamaa kuona vitendo vya ukatili wa watoto na wanawake vinafanywa na watu wenye akili timamu na wanaojua jema na baya.
"Natoa rai kwa jamii kushirikiana kwa pamoja ili kukomesha vitendo hivi mara moja," alisema Mhe.Ngwada.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Iringa, Bi.Tiniel Mbaga amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuhamasisha jamii kushiriki mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili kwani msingi wa vitendo hivyo ni familia, wazazi na walezi ambavyo hufanyika majumbani na wanaofanya ni ndugu wa karibu, wazazi na walezi.
"Hatuawezi kuwa na ulinzi na usalama wa kutosha kwa wanawake na watoto endapo wataendeleza vitendo hivi vya kikatili kwa sababu ukatili huu unafanyika kwa kificho hivyo ulinzi kwa wanawake na watoto unakuwa mdogo kwa sababu hawajitokezi kuleta malalamiko hayo," alisema Mbaga.
Mbaga amesema kuwa ukatili unasababishwa na mambo kama ulevi, mila na desturi, mfumo dume na kutokuwepo kwa hali za kuheshimu watoto majumbani.
Naye Bi.Editha Kayumba ambaye ni Mkaguzi Msaidizi Dawati la Jinsia na Watoto amesema watoto wanafanyiwa ukatili kwa kuajiriwa wakiwa na umri mdogo, kukatishwa shule pia hata kulawitiwa kitendo ambacho kinatengeneza chuki na kisasi kikubwa mioyoni mwao hata kufikia hatua ya kulipa kisasi kwa vitendo walivyofanyiwa nyuma.
Mtumishi wa Mungu wa Kanisa la Kilutheri Tanzania mama Mchungaji Upendo Koko amesema, mimba za utotoni zinakatisha ndoto za watoto , ugomvi katika familia pia ni chanzo, cha ukatili suala la kujithamini binafsi na kujipenda mwenyewe na kusema kila ukatili una kisasi chake.
Maadhimisho hayo yamefanyika tarehe 11/12/2021 yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali ,Watumishi na wananchi wa Manispaa ya Iringa ambapo wataalamu walipata nafasi ya kutoa elimu katika maeneo ya soko kuu, soko la mashine tatu,stendi ya Mlandege,Stendi ya zamani na uwanja wa mlandege Shule ya msingi.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa