Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Mh. Ibrahim Ngwada amekabidhi shilingi Milini 3 kwa Timu ya Lipuli leo tarehe 19.02.2021, kama hamasa kuelekea katika mchezo baina yao dhidi ya Mawenzi Market FC ya Morogoro.
Aidha Mh. Ngwada amekabidhi pesa hiyo kwa mchanganuo wa laki moja kwa kila mchezaji na benchi la ufundi huku akiwatakia heri ya mchezo huo utakaochezwa kesho kwenye majira ya saa kumi jioni
Sambamba na hilo Mh. Ngwada akizungumza na wachezaji hao katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa amesema "sisi kama viongozi tunahitaji kuona timu ya Lipuli inapanda daraja na kwenda kucheza katika Ligi kuu"
"Sisi kama Halmashauri, tupo tayari kuwa mmoja ya wadau, na mimi kama Meya nipo tayari kwa timu hii ya Lipuli kushirikiana nayo ili kuhakikisha inapata mafanikio" Mh. Ngwada alisema
Aidha amesema, yeye kama kiongozi dhamira yake ni kuhakikisha anashirikiana na chama cha mpira wa miguu na uongozi wa Lipuli katika kuifanya timu kuwa na chachu ya maendeleo hasa katika kujiingizia kipato na kupanda kwa daraja
"Jiwekezeni katika michezo ndio ajira yenu, zingatieni mafunzo ipo siku mtafika mbali zaidi ya hapo huku heshima yenu na nidhamu ndio itakayo wapa kufika viwango vya juu zaidi" Hayo yamezungumzwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga akiwa kama mmoja wa aliyeshiriki katika tukio hilo
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Iringa Ndg. Salvatory Ngelela, amempongeza Mstahiki Meya kwa kuifanyia kazi Ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika upande wa Michezo na kutimiza ahadi yake wakati alipokuwa akiomba kura kwa wananchi kuwa angezisaidia timu za mpira wa miguu zilizopo katika Halmashauri yake
Rita Kabati, Mbunge wa Viti Maalum Jimbo la Iringa Mjini naye amewataka viongozi wa Lipuli na mpira wa miguu, wasiache kuwashirikisha changamoto zao ili kama viongozi wajue ni kwa namna gani wataweza kuwasaidia huku akiamini timu ya Lipuli inaenda kupanda daraja katika msimu huu
Mwenyekiti wa Timu ya Lipuli Ndg. Mussa Wanguvu, amemshukuru Mstahiki Meya kwa mchango wake dhidi ya timu ya Lipuli huku akimkabidhi tisheti ya uwananchama wa heshima katika timu yake
"Tunashukuru sana Mstahiki kwa ulichokifanya, na sisi tunakuahidi siku ya kesho kufanya vizuri katika matokeo dhidi ya Mawenzi Market" Mwenyekiti wa Lipuli aliongezea kwa kusema hayo
Kwa upande wake nahodha wa timu ya Lipuli Ndg. Hamis Mroki ameahidi kwa niaba ya wachezaji kuonesha nidhamu, kufanya vizuri mpaka kurudi katika Ligi kuu huku akibainisha moja ya changamoto yao kuwa ni ukosefu wa viatu wakati wa mazoezi.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa