Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Halima Dendego ameshuhudia zoezi la utiaji saini lililofanyika Novemba 15, 2023 katika Uwanja wa Mwembetogwa baina ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Jumuiya ya Wafanyabiashara, Umoja wa Wafanyabiashara Masoko na Shirikisho la Wamachinga Wilaya ya Iringa katika makubaliano ya operesheni safisha mji yenye kauli mbiu ya “IRINGA UCHAFU SASA BASI” inayoratajiwa kuanza tarehe 20/11/2023.
Zoezi hilo limesimamiwa na Mwanasheria wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Ndg. Nicholaus Mwakasungula na kutiwa saini na Mstahiki Meya Mhe. Ibrahim Ngwada na Mkurugenzi Ndg. Kastori Msigala kwa upande wa Manispaa ya Iringa, huku katika Jumuiya ya Wafanyabiashara, Umoja wa Wafanyabiashara Masoko na Shirikisho la Wamachinga Wilaya makubaliano hayo yametiwa saini na Mwenyekiti na Katibu.
Maeneo yanayokusudiwa kufanyika operesheni hii ni Mashine tatu, Miyomboni, Magari mabovu, Zizi, Ipogolo, Mlandege na Kihesa, ikilenga kufanya usafi katika Mifereji na barabara za mji, Maeneo ya masoko, Stendi, Hospitali, Maeneo ya Magereza na Kuondoa Wafanyabiashara holela waliopo vichochoroni.
Ili kukamilisha zoezi hili hatua za awali za kupita na kuwajulisha wafanyabiashara holela kuhama maeneo yasiyo rasmi na kuhamia maeneo rasmi, zitachukuliwa na Kamati inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa Iringa na Kamati ya Usalama Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Iringa na Kamati ya Usalama Wilaya, Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa na Wilaya, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Viongozi wa Umoja wa Wafanyabiashara Masoko na Viongozi wa Shirikisho la Wamachinga Wilaya ya Iringa.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa