Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Halima Dendego amezindua rasmi operesheni ya usafi ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Novemba 20, 2023 yenye Kauli mbiu ya “IRINGA UCHAFU SASA BASI” itakayokwenda kwa siku saba katika Kata zote ndani ya Halmashauri.
Uzinduzi huo umefanyika katika Kata ya Ruaha kwenye maeneo ya Soko la Ipogolo, Soko la Mwagongo na Stendi ya Ipogolo ambapo Mhe. Dendego alipata fursa ya kuongea na wafanyabiashara wadogo wa Soko la Mwagongo na kuwaasa wahamie katika Soko la Ipogolo ili kuepusha usumbufu usio wa lazima wa magonjwa ya mlipuko kutokana na mazingira kuwa machafu na adha ya kushindwa kupita na magari katika eneo hilo kutokana na wao kujenga vibanda vya soko katika eneo la barabara.
“Nawapa siku 10 wote mhamie Soko la Ipogolo kule kuna nafasi nzuri mtauza bidhaa zenu kwa uhuru, mnaona mlivyoziba njia hivi, mama mjamzito akitaka kujifungua hapa atapita wapi?, Ikifika tarehe 30 nisikute mtu hapa kama kuna watu wanachangamoto, walikopa mahali waorodheshe majina yao na walikopa benki gani kila mmoja aandike anadaiwa kiasi gani ili nione cha kufanya” amesema Dendego.
Shughuli zilizofanyika katika uzinduzi ni Kutoa elimu ya usafi kwa wananchi na wafanyabiashara, Kufanya usafi kwenye mitaro na mifereji, pia Kuhamasisha wafanyabiashara wadogo kuhamia katika maeneo rasmi.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Veronica Kessy amewataka viongozi na watendaji kuhakikisha wanasimamia zoezi hili kwa lengo la kuifanya Iringa kuwa safi na maeneo yote ambayo yamesafishwa kubaki yakiwa safi na kuwataka baadhi ya wafanyabiashara ambao bado hawajahamia maeneo rasmi kuhamia maeneo yaliyotengwa na serikali kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Viongozi wa serikali na watendaji wa mitaa hakikisheni zoezi hili linakuwa endelevu katika mtaa wako ili kuacha maeneo yote masafi na pia niwashukuru baadhi ya wafanyabiashara kwa kuwa waelewa na kuhamia katika maeneo rasmi ya kufanyia biashara lakini niwakumbushe kutokufanya biashara holela, endeleeni kuvitoa vitu vyenu na kuhamia pale ambapo tumewatengea vinginevyo Manispaa watafanya kazi yao” Amesema Kessy
Operesheni ya “Iringa Uchafu Sasa Basi” katika Kata ya Ruaha imeongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Katibu Tawala Wilaya, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Viongozi wa Umoja wa Wafanyabiashara Masoko na Viongozi wa Shirikisho la Wamachinga Wilaya ya Iringa.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa