Na Mwandishi Wetu, Iringa
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendiga, amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri za Mkoani humo kusimamia shilingi bilioni 8.6 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa kuhakikisha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Ametoa agizo hilo Novemba 3, mwaka huu wakati akizungumza kwenye kikao na watumishi wa Wilaya ya Iringa na wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kilichofanyika kwenye ukumbi wa Orofea uliopo kata ya Kitanzini mjini Iringa.
Katika kikao hicho, Sendiga alimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha Sh bilioni 8.6 katika Mpango wa Maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19 kwa Mkoa wa Iringa.
"Wakurugenzi hakikisheni fedha hizo mnazisimamia vyema ziweze kutumika kama zilivyokusudiwa na kukamilisha miradi kwa wakati uliopangwa ili kutatua changamoto katika jamii," alisema Sendiga.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amewataka watumishi kumpa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake ili kuleta maendeleo chanya Mkoani hapa.
"Niwaombe watumishi tushirikiane na kila mmoja atimize wajibu wake nami nitawapa ushirikiano wa kutosha kwani sisi tunategemeana katika utekelezaji wa majukumu," alisema Sendiga.
Pia amewataka watumishi kuacha migogoro na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hususani waheshimiwa madiwani na badala yake washirikiane nao katika kutekeleza ilani ya chama hicho tawala.
Katika hatua nyingine, Sendiga amepongeza Mkoa wa Iringa kwa kufanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka 2021 kwa kushika nafasi ya pili kitaifa.
Amesema jitihada zilizofanywa na walimu na kuwawezesha wanafunzi kufanya vizuri katika mtihani huo ziendelee ili Iringa izidi kung'ara kitaifa katika matokeo ya miaka ijayo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mohamed Moyo amewataka wakuu wa Idara na vitengo kuzingatia changamoto zilizotolewa na wasaidizi wao ziwe chachu ya mabadiliko na wakasimamie mipango yote ya Serikali iweze kutekelezeka kwa wakati na kuleta tija.
Awali akijibu maswali ya baadhi ya watumishi Sandiga alisema amezichukua changamoto hizo ikiwamo kucheleshwa kwa stahiki zao na ucheleweshwaji wa kupanda madaraja kwamba atahakikisha zinapatiwa ufumbuzi wa haraka.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa