Kamati ya Fedha na Uongozi Halmashauri ya Manispaa ya Iringa chini ya Diwani wa Kata ya Mkwawa, Mhe. Amri Kalinga imekagua maeneo mbalimbali ya biashara katika Kata ya Ruaha.
Mhe. Kalinga akishirikiana na wataalamu kutoka Manispaa ya Iringa pamoja na viongozi wa eneo husika wamekagua biashara hizo Mtaa wa Ipogolo, Kata ya Ruaha. Huku lengo kuu la ziara ni kukagua Leseni za biashara, Ushuru wa huduma, Kutathmini utekelezaji wa bei elekezi ya sukari kama ilivyopangwa na serikali na Ukusanyaji wa ushuru wa taka.
Katika ziara hiyo wajumbe hao walipata fursa ya kutembelea baadhi ya wafanyabiashara waliopo eneo hilo na kukagua zaidi ya biashara 30 ikiwemo Maduka ya mahitaji ya nyumbani, Duka la nyama, Maduka ya pombe (grocery), Nyumba za kulala wageni, Saluni za kike na kiume, Ofisi za huduma za pesa, Gereji na pamoja na Migahawa.
Timu hiyo imebaini kuwa zaidi ya asilimia 80% ya wafanyabiashara eneo hilo hawana leseni ambapo kuna ambao hawajakata kabisa na wengine leseni zao zimekwisha muda wake. Pia zaidi ya asilimia 90% ya wafanyabiashara eneo hilo hawalipii ushuru wa huduma (service levy).
"Kwa wale ambao hamna leseni, pia hamlipii ushuru wa huduma (service levy) pamoja na ushuru wa taka hakikisheni mnakwenda Halmashauri kupata utaratibu wa malipo ili kuepusha usumbufu. Na baada ya malipo hakikisheni mnaweka hati za malipo kwenye biashara zenu ili ukaguzi unapofanyika iwepo tayari". Amesema Kalinga.
Aidha, Katika ukaguzi wa bei ya sukari timu hiyo haikufanikiwa kupata bei halisi inayotumika kwa wafanyabiashara hao. Kwani maduka waliyofanya ukaguzi hakukuwa na sukari. Na hiyo imepelekea kutathmini kuwa huenda wafanyabiashara hao wamekuwa wakiuza bidhaa hiyo kwa bei ya juu ambayo haijaelekezwa na serikali.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Mhe. Ibrahim Ngwada baada ya kupata ripoti ya timu zote za ukaguzi wa biashara kutoka Kata mbalimbali za Manispaa ya Iringa ametoa rai kwa wajumbe wa Kamati hiyo washirikiane pamoja na Viongozi wa mitaa kufanya ukaguzi wa biashara mara kwa mara ili kuongeza mapato ya Halmashauri.
"Tuwe na karatasi ambayo itatambua jina la mfanyabiashara, eneo analofanyia biashara, pamoja na namba ya simu mwisho wa siku tutawasilisha kwenye Kamati kwa ajili ya ufuatiliaji wa mapato". Amesema Ngwada.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Ndg. Kastori Msigala ameshukuru kwa kikao hicho na kuahidi kuwa yale yalioahidiwa yatatekelezwa.
Ziara hiyo imehusisha pia ukaguzi wa maendeleo ya miradi ya Ujenzi wa Ukumbi wa Welfare eneo la Kitanzini unaokisiwa kuwa na thamani ya Shilingi Milioni 44 pamoja na ukamilishaji wa Ujenzi na Miundombinu Stendi ya Igumbilo ambapo ilihusisha timu nzima ya Kamati ya Fedha na Utawala.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa