Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Mhe. Ibrahim Ally Ngwada amewataka wamiliki wa vituo binafsi pamoja na watoa huduma za umma wawe waaminifu na waadilifu hasa katika kusimamia maadili na kanuni zilizowekwa katika kazi zao.
Ameongea hayo katika tukio la utiaji saini wa mikataba baina ya Serikali na Sekta binafsi za afya Mjini Iringa, amesema kuwa vituo binafsi vina mchango mkubwa katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi,hivyo mikataba hiyo inasainiwa kwa lengo la kuboresha huduma za afya baina ya vituo binafsi na Serikali na kuwataka wazingatie mwongozo uliowekwa ili kuboresha huduma hizo.
"Mnachokifanya nyinyi mnaisaidia Serikali, najua nyie ni sehemu ya watoa huduma kwenye jamii yetu, tukisema kuwa huduma zote zitolewe katika vituo vya afya vya Serikali uwezo wa kuhudumia watu wote unakuwa mdogo ". Amesema Ngwada.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Dkt. Godfrey Mbangali ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Manispaa amesema kuwa Halmashauri ina jukumu la kusimamia makubaliano ya mkataba huo yaweze kusainiwa na kutekelezwa ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
"Sisi Manispaa ni walezi wa hivi vituo, tunawalea ili huduma ziweze kutolewa kwa wananchi lengo letu ni kuona huduma za afya zinatolewa kwa usahihi Boresheni huduma zenu, lakini pia boresheni mazingira". Amesema Mbangali.
Aidha, baadhi ya wamiliki na wawakilishi wa vituo vya afya na zahanati wamesema kuwa mkataba huo una manufaa kwao kwani utasaidia katika kusimamia na kutekeleza utendaji kazi ili kuleta ufanisi wa vituo vyao.
Jumla ya vituo vya Umma na Binafsi (17) vinavyohusika na utoaji wa huduma za Afya Iringa vikimemo Marie Stopes, Imecc Hospital, Aghakhan Polyclinic, Cosmopolitans Hospital, Dream Dispensary, Ipogolo Rc na vingenevyo vimesaini mkataba huo chini ya mwongozo wa Wizara ya afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto katika ukumbi wa Manispaa ya Iringa January 30 2024.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa