“ Tunaomba wafanyabiashara wote wanaofanya biashara za magenge mitaani hasa katika Kata ya Kihesa, waje wote katika soko la Ngome kwani nafasi zipo na kuendelea kufanya biashara mitaani inasababisha soko la ngome kukosa wateja”
Ombi hilo limetolewa na Bi, Veronica Mwalongo mfanyabishara wa soko la Ngome baada ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Ndugu Happiness Seneda kufanya ziara ya kutembelea soko la ngome pamoja na miradi mbalimbali ya Maendeleo ndani ya Manispaa ya Iringa.
Amesema imekuwa ni ngumu kufanya biashara katika Soko la ngome kwasababu wafanya biashara wa magenge bado wapo mitaani hivyo Soko hili kukosa mvuto.
Akitoa maelekezo Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Bi, Happinesi Seneda amesema uongozi wa Manispaa ya Iringa uhakikishe wamiliki wote wa magenge yaliyo mitaani wanahamia katika soko la ngome. Pia Manispaa iwasiliane na SUMATRA ili ipangwe njia ya mabasi kupita katika soko hilo ili kuwarahisishia wateja wanaokuja kununua bidhaa katika soko ilo.
Akitoa ufafanuzi Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa Ndugu Omary Mkangama amesema kuwa Manispaa ya Iringa imepanga soko hilo la Ngome kuwa soko la Matunda ya jumla hivyo magari yote ya matunda yatatakiwa kushusha matunda katika soko la ngome na baadae wachuuzi wadodo wadogo watanunua na kusambaza katika masoko mengine.
Sekretarieti ya mkoa wa Iringa imefanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Manispaa ya Iringa. Miradi iliyotembelewa ni mradi wa ujenzi wa vyoo kwa shule ya msingi Azimio na Umoja, ujenzi wa shule ya Mivinjeni, shule ya nduli pamoja na Soko la ngome
Aidha katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Bi, Happinesi Seneda ameuomba uongozi wa Manispaa ya Iringa kwa kushirikiana na uongozi wa Kata ya nduli, kuhakikisha wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule hiyo basi wanafika shuleni hapo hata kama hawana sare. Kwani uwiano wa watoto waliopelekwa shuleni hapa na watoto walio anza masomo hauwiani.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa