Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imefanya zoezi la usaili kwa walioomba nafasi ya kazi ya muda ya Sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 23. 2022.
Raymond Nyenza ni Mratibu wa Sensa Manispaa ya Iringa amesema usaili unafanyika siku mbili (2) kuanzia tarehe 20-21/7/2022 ambapo umewahusisha makarani wa Sensa,Wasimamizi wa Maudhui na wasimamizi wa TEHAMA.
Nyenza amesema wasimamizi wa TEHAMA wanafanya usaili huo katika ngazi ya wilaya ambapo watafanyia usaili ofisi kuu katika ukumbi wa Manispaa ambapo Makarani wa Sensa na wasimamizi wa Maudhui wanafanyia usaili katika ofisi za Kata zilizopo Manispaa ya Iringa kuanzia saa 3.00 asubuhi.
Nyenza amesema wamejiandaa vizuri kuhakikisha zoezi hilo muhimu linaenda vizuri bila changamoto zozote na kuwa muitikio umekuwa mkubwa kwani idadi ya waombaji wote ni zaidi ya watu elfu nne (4000)
Aidha Nyenza amewataka wasailiwa wote kujiamini,kujibu maswali kwa usahihi ili waweze kufaulu katika usaili huo na hatimaye kwenda kufanya kazi hiyo kwa usahihi kwa maslahi mapana ya Taifa letu.
Bi.Christina Mfinanga na Bw.Johnbosko Emmanuel ni wasailiwa wamesema waliomba kazi hiyo kwa kuwa wana sifa,uwezo na wanaamini watafanya vizuri katika usaili huo hatimaye kuchaguliwa kutekeleza majukumu yatakayokuwa mbele yao kwa mujibu wa mafunzo watakayopewa .
Sensa ya watu na makazi hufanyika kila baada ya miaka kumi (10) kwa lengo la kujua takwimu sahihi za watanzania ili kuweza kupanga mipango ya maendeleo kutokana na takwimu hizo, kwa mara ya mwisho Sensa ya watu na makazi ilifanyika mwaka 2012.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa