Wananchi wa Manispaa ya Iringa wametakiwa kuendelea kutunza mazingira kwa kuhakikisha wanapanda miti katika kila maeneo wanayoishi.
Hayo yamesemwa leo Januari 19. 2022 na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Mhe. Ibrahim Ngwada katika uzinduzi wa upandaji miti kiwilaya uliofanyika katika shule ya msingi Nyumbatatu iliyopo Kata ya Ilala.
Aidha zoezi hilo limehusisha washiriki mbalimbali wakiwemo wadau wa mazingira Envibright, Chuo kikuu Katoliki Ruaha, Madiwani na wananchi, ambao kwa umoja wao walijitokeza kupanda miti kwenye maeneo mbalimbali ya shule hiyo .
"Niwapongeze wadau wa usafi kwa ushiriki wa zoezi la leo na ninaahidi kutoa ushirikiano mimi na Madiwani wenzangu pale mtakapotuhitaji katika suala lolote la utunzaji wa mazingira" Mhe Ngwada alisema
Hata hivyo Mh. Ngwada amemtaka Mkurugenzi kutoa ushirikiano kwa wadau wa mazingira na kuendelea kusambaza miti katika maeneo yote ya Manispaa zikiwa ni jitihada za kutunza mazingira
Naye Mhe. Conrad Mlowe ambaye ni Diwani wa kata ya Ilala ambapo shule ya Msingi Nyumbatatu ilipo amemshukuru Meya wa Manispaa pamoja na wadau wa mazingira kushiriki katika zoezi hilo na kuahidi miti waliyoipanda wataitunza ipasavyo.
Awali akiongea mbele ya mgeni rasmi Prof Pius Mgeni, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Katoliki Ruaha(RUCU) amewataka wananchi kujenga tabia ya kukata mti na kupanda mti kwani kwa kufanya hivyo wataweza kurithisha vizazi vijavyo Dunia yenye mazingira safi .
Katika zoezi hilo la upandaji wa miti jumla ya miche 100 ya matunda ya parachichi ilipandwa ambapo wanachi waliojitokeza walipewa kila mmoja mche mmoja kwa ajili ya kupanda katika maeneo yao wanayoishi.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa