“Kiongozi bora ni yule mwenye sifa na uwezo wa kuwaongoza wananchi, lakini pia ni yule ambaye sera na mipango yake inaakisi uhalisia wa changamoto za wananchi katika maeneo yao.”
Kauli hiyo imetolewa na Kiongozi wa Kitaifa wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024, Ndg. Godfrey Mzava wakati akizungumza na wananchi wa Iringa katika eneo la bustani (Garden) iliyopo Kata ya Gangilonga Manispaa ya Iringa na kutoa ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Mwaka 2024.
Mzava amesema, uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafanyika hivi karibuni nchi nzima hivyo wananchi wachague kiongozi mwenye vitendo vizuri kwenye jamii, wanaokubalika lakini pia wenye sifa njema na wasichague viongozi wala rushwa na mafisadi.
Moja ya Askari Mkimbiza Mwenge Ndg. Makwaya Joseph ametoa salamu za mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 kwa niaba ya Kiongozi Mkuu wa Kitaifa na kusema ni vyema wananchi washiriki katika mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kupata viongozi bora na wenye sifa.
"Wananchi mna wajibu wa kufanya mambo yafuatayo ili kuweza kutimiza uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Moja, kujitambua mwenyewe kama unaona una vigezo na sifa za kuwa kiongozi jambo lingine, twende tukachukue fomu kwa wingi kwenye vyama vyetu vya siasa na muhudhurie kampeni kwa wingi ili kusikiliza sera za viongozi hao, msipokee wala kutoa rushwa". Amesema Makwaya.
Aidha Makwaya ametoa rai kwa wananchi kuwa ifikapo siku ya uchaguzi wajitokeze kwa wingi kupiga kura ili kuweza kupata kiongozi bora.
Afisa Uchaguzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Ndg. Bernard Mwaituka amesema Manispaa ya Iringa inatarajia kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mpaka sasa imekwishaandaa vituo 199 vya kuandikisha wapiga kura, pia vituo 358 vimeandaliwa kwa ajili ya kupigia kura pamoja na kuanza maandalizi ya awali ya kufanikisha shughuli za uchaguzi.
Mwaituka ameendelea kutoa elimu ya uchaguzi kupitia vyombo vya habari na kuhamasisha wananchi kujiandaa kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Wakimbiza Mwenge Kitaifa na wananchi waliojitokeza kwa wingi kuupokea Mwenge wa uhuru walikongwa mioyo yao kutokana na umahiri wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Ipogolo wakiongozwa na mwalimu wao walivyoonyesha igizo la uhamasishaji wa wananchi kujitokeza kupiga kura na namna wananchi watakavyopiga kura katika uchaguzi ujao.
#tume ya uchaguzi_TZ
#Tume Huru ya Taifa ya uchaguzi
#ofisiyawazirimkuu
www.kazi.go.tz
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa