Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Kheri James amewataka wananchi kuwa na utaratibu wa kuwasilisha changamoto wanazozikuta kwenye maeneo mbalimbali ya huduma ili serikali iweze kuchukua hatua za kuboresha changamoto hizo.
Mhe. Kheri amesema hayo katika Mkutano na Wananchi wa Kata ya Ilala, uliofanyika siku ya tarehe 03/06/2024 katika Ofisi ya Kata ambapo amesema kuwa serikali hii ni serikali ya wananchi, inachaguliwa kwa kura za wananchi na inaongozwa kwa kodi za wananchi. Hivyo serikali inafanya utaratibu wa kuwasikiliza wananchi. Na ndio sababu katika maeneo ya huduma kama vile hospitali, ofisi za umma, polisi, taasisi za elimu na kwingineko kuwa serikali imeweka namba za mawasiliano pindi mwananchi anapokutana na kero zozote zile wawasiliane na uongozi kwa hatua zaidi.
"Ukienda hospitali, utakuta tumekuandikia pale namba za Mganga Mkuu wa Wilaya, Mganga Mfawidhi, na wengine wote tukiwa na dhamira ya unapofika hospitali, ukaona mwenendo wa huduma si mzuri. Unatakiwa kuwasiliana na sisi kupitia namba hizo, ili tujue hapo ulipofika changamoto ni nini, unasumbuliwa na nani ili tuchukue hatua za kuboresha changamoto hizo". Amesema Kheri.
Katika ziara hiyo ya kata ya Ilala Mkuu wa Wilaya amekagua miradi miwili ambayo ni ujenzi wa choo chenye matundu manne kilichojengwa eneo la Soko la Ilala ambalo limegharimu kiasi cha Shilingi Milioni 9, pamoja na Ujenzi wa Madarasa katika Shule ya Sekondari Mlamke.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Mhe. Ibrahim Ngwada amesema kuwa serikali inafanya jitihada mbalimbali kuboresha huduma kwa wananchi kama vile Ujenzi wa barabara za mitaa kwa kiwango cha lami, Ujenzi na Uboreshaji wa Shule za Msingi na Sekondari pamoja na Ujenzi wa Zahanati na
Vituo vya Afya.
Pia amesema katika kipindi hiki Halmashauri imepokea zaidi ya Shilingi Bilioni 2 kwa ajili ya uboreshaji wa hospitali ya Wilaya - Frelimo. Mpaka sasa hospitali ina Wodi za Wanaume na Wanawake, Jengo la kujifungulia, Huduma ya Mama na Mtoto pamoja na Jengo la kuhifadhia maiti.
Akiwasilisha taarifa katika Mkutano huo, Diwani wa Kata ya Ilala Mhe. Conrad Mlowe amesema serikali imekamilisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kwa wananchi wa Ilala, Ujenzi wa madarasa, pia imetafuta eneo la soko ambapo sasa hivi kufikia hatua ya ujenzi wa choo, kwa niaba ya wananchi ameiomba serikali kujenga uzio kwa Shule ya Sekondari Mlamke kwaajili ya usalama wa wanafunzi kwani mazingira si rafiki.
Mpaka sasa Mhe. Kheri ameshafanya ziara katika Kata ya Nduli, Mwangata, Mkimbizi, Mtwivila na Ilala huku lengo kuu la ziara hiyo ni Ukaguzi wa miradi ya Maendeleo ya Kata, Kuhamasisha Shughuli za Maendeleo na Kuwasikiliza Wananchi.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa