Imeelezwa kuwa upotoshwaji wa baadhi ya watu kuhusu chanjo ya UVIKO-19 ndiyo sababu kubwa ya wananchi kusuasua kujitokeza kupata chanjo hiyo.
Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Mohamed Moyo katika Ukumbi wa mikutano wa Manispaa wakati wa kikao cha kamati ya Afya ya Msingi ambayo iliwajumuisha wajumbe na wadau mbalimbali wa afya.
Mh. Moyo amewataka wajumbe wa kikao hicho kuwa makini kupokea elimu inayotolewa na wataalamu na kuwa mabalozi wazuri kuhamasisha jamii iweze kuchanja kwa hiyari.
Aidha Mhe Moyo ametoa rai kwa wananchi wa Manispaa kuunga mkono jitihada za Serikali za kudhibiti ugonjwa wa UVIKO-19 kwa kuendelea kuzingatia miongozo inayotolewa na wizara ya Afya.
Wakizungumza baada ya mafunzo hayo baadhi ya wajumbe na wadau waliohudhuria kikao hicho walisema Taasisi za dini, Wanasiasa na vyombo vya habari vikitumika ipasavyo vinaweza kusaidia katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo pamoja na chanjo kwa kuwa wana Rasilimali watu.
Naye Mratibu wa chanjo Manispaa ya Iringa bwana Khamis Omary amesema chanjo ya UVIKO-19 ni kinga pia inasaidia mtu akipata Maambukizi asipate madhara makubwa.
Viongozi wa dini wa Manispaa wamesema wako tayari kutoa ushirikiano kwa wataalamu wa afya kutoa elimu ya ugonjwa huo kwenye nyumba za ibada hivyo wataalamu wawape ratiba ili waendelee kutoa elimu mara kwa mara kwa kufanya hivyo itasaidia kuleta uelewa wa kutosha katika jamii.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa