"Wanawake tuzikamate nyumba, lakini pia tusiache kujishughulisha ili kuepukana na kunyanyasika kwani naamini sisi wanawake tukijiimarisha kiuchumi basi tutaheshimika"
Hayo yamezungumzwa leo na Mhe. Rita Kabati, Mbunge wa Viti Maalum Jimbo la Iringa Mjini akiwa Mgeni rasmi katika Kongamano la Wanawake kuelekea maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani ifikapo tarehe 8 Machi mwaka huu
Aidha Mhe. Rita Kabati amewataka wanawake hao kuendelea kusaidiana katika changamoto wanazokutana nazo na sio kushirikiana wakati wa raha tu huku akiwataka kujitokeza katika nafasi mbalimbali za uongozi zinapojitokeza
Nae Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Iringa Ndugu. Nicolina Lulandala amewaomba wanawake hao kujiwekea utamaduni washiriki katika masuala mbalimbali wanayoshirikishwa ili kuonesha wanauwezo pia amewataka kuendelea kushikamana wao kwa wao kwani kupitia umoja wao utaweza kuleta mabadiliko chanya katika familia zao,jamii na Taifa kwa ujumla
Sambamba hayo, pia kongamano hilo limeambatana na uwasilishwaji wa mada mbalimbali zilizofundishwa kwa wanawake waliohudhuria kama hamasa katika kuelekea siku hiyo kwa ujumbe usemao wanawake katika uongozi chachu kufikia dunia yenye usawa
Mada zilizowasilishwa ni pamoja na Ujasiriamali, Wanawake na Uongozi, Mirathi, Ndoa, Ukatili wa kijinsia, CHF Iliyoboreshwa, Elimu ya fedha, Lishe pamoja na Masuala ya Binti
Dkt. Given Msomba kutokea Chuo Kikuu cha Iringa ambae ni muwasilishaji wa mada ya Wanawake na Uongozi amewataka wanawake hao kujijengea maamuzi binafsi yenye hamasa ya kuleta mabadiliko na sio kubaki nyuma na kutegemea maamuzi yote kutoka kwa mwanaume hali ambayo itaonyesha kuwa ishara ya sifa ya mwanamke kiongozi bora
Tiniel Mbaga, Afisa Utawi wa Jamii Manispaa ya Iringa amewataka wanawake kupinga ukatili dhidi yao na watoto wao pia kuyatolea taarifa katika vyombo vya kisheria ili kupata msaada kwa haraka mara baada ya matukio hayo kutokea
Kwa upande wake Bi. Flora Bruno ambaye ni Mratibu wa bima ya afya ya CHF Iliyoboreshwa Manispaa ya Iringa, amesema ili kuyafikia maendeleo kiujumla, afya ni jambo la kuzingatia hivyo ametoa elimu juu ya bima hiyo na amewataka wanawake hao kuziboresha afya zao na familia zao kwa kujiunga katika mfuko huo.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa