Wito umetolewa kwa wataalam kutekeleza masuala ya Lishe katika jamii ili kupunguza na kutokomeza kabisa tatizo la utapiamlo katika Manispaa ya Iringa.
Wito huo umetolewa leo tarehe 20.5.2021 na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Mhe. Ibrahim Ngwada ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Afya kwenye Tathmini ya Mikataba ya Lishe ambayo hufanyika kila robo lengo likiwa kuangalia utekelezaji wa viashiria vya Mkataba vilivyotekelezwa katika Kata zote
Mhe.Ngwada alieleza kwamba lazima agenda ya lishe ijadiliwe kwa weledi kwenye vikao vya maendeleo ya kata, alisisitiza watoto wote chini ya miaka mitano wapimwe hali zao za lishe kwenye siku za maadhimisho ya afya na lishe ili kuwaibua mapema wenye utapiamlo wapate matibabu kwa wakati. Aliagiza uongozi wa kata uweze kuwasimamia wahudumu wa afya ngazi ya jamii watembelee kaya na kutoa elimu ya lishe pia kuhakikisha taarifa zote za lishe zibandikwe kwenye mbao za matangazo
Mwisho aliweza kueleza kwamba shule zote za msingi na sekondari zilizopo Manispaa ya iringa ziwe na bustani za mboga na matunda pamoja na kuhakikisha kwamba wanafunzi wote wanakula chakula wakiwa shule.
Anzael Msigwa Afisa lishe wa Manispaa amesema mafanikio makubwa yaliyopatikana ni pamoja na usimamizi mzuri wa viashiria vya mkataba kutoka kwa wataalam waliopo kwenye kata pamoja na wahudumu wa afya ngazi ya jamii kutekeleza kwa wakati shughuli za lishe
Pia amezitaja changamoto kuwa ni kuchelewa kuibuliwa kwa watoto wenye utapiamlo katika Mitaa na Kata hivyo kufanya kufika kwenye vituo vya Afya wakiwa na hali mbaya.
Eliud Mvela ni mhe.Diwani Kata ya Mkimbizi ameshauri watendaji na wahudumu wa afya msingi kushirikiana kwa pamoja kuibua watoto wenye utapiamlo ili waweze kupata tiba kwa wakati.
Kikao hicho kimewahusisha wadau mbalimbali wa Lishe wakiwemo Waheshimiwa Madiwani, Wakuu wa Idara na vitengo,watendaji wa Kata Maafisa maendeleo ya jamii, wadau wa lishe ni pamoja na Papa yohana 23,Lishe Endelevu. Mbogamboga na Matunda,Save the Children,Tahea, Alamano na Call Africa.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa