Mkuu wa Wilaya ya Iringa ndugu Richard Kasesela amewataka watendaji kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha kodi mbalimbali zinatolewa kwa mujibu wa sheria taratibu na kanuni zilizowekwa ili kufikia malengo ya ukusanyaji waliyojiwekea
Kauli hiyo ameitoa leo tarehe 11/2/2021 kwenye kikao cha kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Manispaa ya Iringa kwa lengo la kupitia bajeti ya mwaka 2021/2022
Aidha Kasesela amesema watendajii wanajukumu kubwa kuhakikisha kodi mbalimbali zinakusanywa kwa wakati na bila bugudha na ameainisha kodi zilizorudishwa kukusanywa na Halmashauri ni pamoja na Kodi ya majengo,kodi ya mabango ambazo awali zilikuwa zikikusanywa na mamlaka ya mapato Tanzania(TRA)pamoja na kuhakikisha wafanyabiashara wote wanakuwa na vitambulisho vya wajasiriamali awamu ya tatu ambavyo vitaanza kuuzwa hivi karibuni
Kasesela amesisitiza katika bajeti ya 2021/2022 ipo haja ya kuangalia changamoto ya usafiri kwa watendaji na kuhakikisha suala hilo linaingia kwenye bajeti ili kurahisisha utendaji kazi wao na kuwafanya wafanye kazi kwa weledi
Kuhusu Sekta ya elimu Kasesela amewapongeza walimu kwa kufanya kazi kwa bidii hivyo kuufanya Mkoa wa Iringa kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya kidato cha pili na kidato cha nne
Ameshauri bajeti ijayo katika Idara ya Elimu Sekondari izingatie suala la kambi za wanafunzi wa kidato cha nne angalau waweze kukaa kwa kipindi kisichopungua miezi miwili ili kuongeza ufaulu kwa mwaka 2021 katika Mkoa wa Iringa
Said Lubeya ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya amesema anawapongeza watumishi wote wa Halmashauri kwa kukusanya mapato zaidi ya lengo ililojiwekea na kusema pamoja na upungufu wa wafanyakazi uliopo bado Halmashauri imefanya vizuri katika Usafi wa mazingira,Mitihani,ukusanyaji wa mapato na shughuli zingine za kiuchumi hivyo kuwaletea maendeleo wananchi wake
Lubeya ameahidi kushirikiana na watendaji katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi pamoja na Madiwani wakiongozwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa mhe. Ibrahimu Ngwada kuhakikisha wanaonyesha tofauti ya utawala wa CCM na CHADEMA
Mstahiki Meya Manispaa mhe.Ibrahim Ngwada amemshukuru Mjumbe wa Halmashauri kuu CCM Taifa (MNEC) Salim Abri Asas kwa kufanya marekebisho ya jengo la ofisi yake na kusema kuna haja ya viongozi wote wa chama na Serikali kutambua kazi kubwa inayofanywa na MNEC katika jamii na kumpongeza kwa moyo wa kujitoa kwa ajili ya wananchi
Omary Mkangama ni kaimu Mkurugenzi ameahidi kuyapokea marekebisho yote yaliyofanywa katika mapitio ya bajeti hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi mapema iwezekanavyo
Kikao cha kamati ya Ushauri ya Wilaya hufanyika mara moja kwa mwaka na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, vyama na Serikali,Taasisi za kiraia pamoja na wakuu wa Idara na vitengo na watendaji wa Kata.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa