Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mhe. Kheri James amewataka watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kuzingatia miongozo na kanuni za utumishi wa umma katika utendaji kazi pindi wanapokuwa katika majukumu yao.
Akizungumza hayo katika ukumbi wa Manispaa amesema ili Halmashauri ifanye kazi vizuri watumishi wanapaswa kuzingatia mambo muhimu matano ambayo ni Utawala wa Sheria, Haki, Usawa, Maendeleo pamoja na Umoja na Mshikamano.
“Ili tufanye wajibu wetu vizuri jambo la kwanza ni kufahamu kwamba nchi hii inaongozwa kwa mujibu wa katiba, sheria, kanuni, taratibu, miongozo, maamuzi ya vikao na maelekezo ya viongozi yasiyokinzana na utawala wa sheria pamoja na mahitaji ya wakati. Huu ndio msingi wa utawala wa nchi yetu, kila mmoja anapofanya majukumu yake kama ni maneno au matendo ajiulize ni kwa kiwango gani yameheshimu mambo haya yote ". Amesema Kheri.
Aidha, Kheri amewaonya watumishi juu ya tabia binafsi zisizofaa miongoni mwao kama vile uongo, uzushi, majungu na kujipendekeza kwa wakubwa kwani inapelekea kuathiri mfumo wa utendaji kazi wa Serikali lakini pia zinashusha heshima ya Taasisi.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Wakili Nicholaus Mwakasungula amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kufika mahali hapo ili kufahamiana na watumishi na pia kwa nasaha na ushauri aliotoa kwa watumishi. Ameahidi kusimamia utekelezaji wa maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Wilaya.
Mhe. James amefanya kikao na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kwa lengo la kufahamiana na watumishi kwani amewasili Mkoani Iringa hivi karibuni mara baada ya mabadiliko ya uongozi yaliyofanywa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu akitokea Wilaya ya Mbulu.
Aidha kauli mbiu ya Mkuu wa Wilaya Mhe. Kheri James inasema “Iringa Imara, Tutaijenga kwa Umoja na Uwajibikaji”.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa