Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Komred Kheri James amewashauri Wazazi kutenga muda wa kukaa na watoto wao na kujenga mahusiano mazuri ya kirafiki na ya ukaribu ili kuwaweka karibu watoto na kuwafanya wawajue wazazi wao vizuri.
Ametoa ushauri huo wakati wa kuweka Jiwe la Msingi katika Shule mpya ya Sekondari ya Kwavava iliyopo Kata ya Kitwiru Halmashauri ya Manispaa ya Iringa huku akiwaasa kina mama wanaolea watoto peke yao kuepuka kuvunja mahusiano baina ya baba na watoto kwani kufanya hivyo ni kuwanyima watoto haki yao ya msingi ya malezi.
“Malezi bora ya watoto yanatoka kwa wazazi wa pande zote mbili, wakati akinamama wanawafundisha watoto huruma na upendo lakini ujasiri na mapambano hujifunza kutoka kwa akinababa na hii huwafanya watoto kuwa watu bora zaidi katika maisha yao na kwamba watoto ni watu ambao tutakuwa nao katika nyakati zote” Amesema Komred Kheri
Aidha amewataka watoto ambao ni wanafunzi wa shule hiyo kusoma kwa bidii sana na kujipanga kufaulu katika masomo yao, kwa kuwapenda sana walimu wao na kufanya hivyo itawasaidia kulipenda somo la mwalimu husika tofauti na hivyo ni mwanzo wa kuwapelekea kufeli, pia amewashauri kujijengea ujasiri wa kufuatilia kwa kuwaomba msaada walimu wao katika masomo wasiyoyaelewa.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kwavava Ndg. Vick Kasanga, amesema Mradi huo umegharimu zaidi ya Tsh. Milioni 500 na Malengo ya Mradi huo wa ujenzi wa Shule ulianza kutekelezwa Agosti 2023 na kukamilika kwa asilimia 98, pamoja na kuboresha mazingira ya kujifunza na kujifunzia, kupunguza msongamano darasani na kusogeza karibu huduma ya elimu kwa jamii.
Mwl. Kasanga amebainisha kuwa Shule ya Sekondari ya Kwavava imeanza kutoa elimu kwa Mwaka wa masomo 2024 kwa kidato cha kwanza na hadi sasa wana jumla ya wanafunzi 105 na walimu watano (5)
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kitwiru Mhe. Hamza Mwamhehe amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi wa Kata hiyo kwani katika kipindi kifupi cha Uongozi wake ametoa fedha nyingi katika Sekta ya Elimu na Afya.
Uwekaji wa Jiwe la Msingi umeshuhudiwa na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi ngazi ya Kata, Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya, Kamati ya Ujenzi, Walimu, Wanafunzi, Watendaji wa Mitaa na Mtendaji wa Kata pamoja na wazazi.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa