Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega ametoa pongezi kwa viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Daraja, Bweni pamoja na Stoo ya dawa miradi ambayo itawanufaisha wakazi wa Iringa.
Waziri Ulega ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na wananchi wa Iringa katika Mkutano wa hadhara, uliofanyika katika Uwanja wa shule ya Msingi Muungano iliyopo Kata ya Mwangata Tarehe 17.09.2024.
"Yanapofanywa mazuri lazima tupongezane, hiyo inatoa kasi zaidi ya kufanya vizuri zaidi, nawashukuruni sana wanaIringa, nimekagua, nimefungua na kuweka mawe ya msingi katika miradi ya maendeleo ya ujenzi wa Daraja Kigonzile, Bweni la Mawelewele na Stoo ya Dawa Hospitali ya Frelimo. Miradi hiyo inakwenda kutatua kero na changamoto za watu. Hakika nmeridhia, mmefanya vizuri. Nawapongeza sana. Ntazifikisha salamu zenu kwa Mheshimiwa Rais". Amesema Ulega.
Aidha, Ulega amewaasa wananchi kuchagua viongozi bora, wachapakazi, wazalendo, wabunifu na wenye uwezo wa kusimamia maendeleo ya watu katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwishoni mwa Mwezi Novemba 2024. Vilevile wahakikishe wanaendesha uchaguzi kwa amani na utulivu ili kulinda amani ya Nchi yetu.
Wakati huo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe, Peter Serukamba ametoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu kwa kuleta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi kwani anapambana katika kuondoa maadui watatu katika Nchi ya Tanzania ambao ni "Ujinga, Maradhi na Umaskini". Ndio maana amejikita kuleta fedha hasa katika miradi ya Elimu kwa ajili ya kufuta Ujinga, miradi ya Afya kwa kuondoa maradhi pamoja na kutoa mikopo kwa kina mama,watu wenye ulemavu na vijana kwa lengo la kuondoa umaskini.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini Mhe, Jesca Msambatavangu ameushukuru uongozi wa awamu ya sita kwa kuzindua bohari ya Dawa ya wilaya(Frelimo) ikiwa ni mkakati wa kupunguza malalamiko na kutatua changamoto ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwani kutokana na utunzaji wa dawa kwenye bohari hiyo itakuwa njia bora kwa zahanati na vituo vya afya vilivyopo kwenye Halmashauri yetu kuweza kupata dawa na vifaa tiba kwa wakati na kwa urahisi hivyo kurahisisha huduma za matibabu kwa wananchi wa Iringa.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM ) Wilaya ya Iringa, Mjini Ndg. Hassan Makoba amesema kuwa ziara hiyo ya Mheshimiwa waziri ni pamoja na kukamilisha ilani ya CCM 2020-2025 ambapo amekuja kuthibitisha kama ilani hiyo imetekelezwa na kuhakikisha zile fedha nyingi ambazo zinaletwa na Mheshimiwa Rais kwenye Hlalmashauri na Mkoa wa Iringa kupitia usimamizi wa Madiwani na wabunge zimekwenda kutatua kero na kutekelezwa kwa vitendo ikiwemo ujenzi wa Daraja, Bweni na Stoo ya dawa.
Miradi mitatu iliyozinduliwa na kuweka jiwe la msingi na waziri huyo ni Ujenzi wa Daraja la Kigonzile lenye (urefu wa mita 10.8) ambao umegharimu Shilingi Milioni 119, Bweni la Shule ya Sekondari Mawelewele Shilingi Milioni 112 na Stoo ya kuhifadhi dawa Hospitali ya Frelimo uliogharimu Shilingi Milioni 160. Miradi hiyo imeshakamilika kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa Iringa
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa