ZAIDI YA MITI 200 YAPANDWA KITUO CHA AFYA MKOGA
Katika kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani, wanawake wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wametumia fursa hiyo kupanda miti zaidi ya 200 siku ya Jumatano tarehe 06 Machi, 2024 katika kituo cha afya Mkoga kilichopo kata ya Isakalilo Mjini Iringa.
Akizungumza katika zoezi hilo la upandaji Miti, Mratibu wa sherehe ya siku ya Mwanamke Duniani wa Manispaa ya Iringa, Ndg. Sunday Mtamakaya amesema kabla ya kilele cha Maadhimisho ya sherehe ya Mwanamke Manispaa ya Iringa huwa inaandaa shughuli mbalimbali. ambapo kwa mwaka huu walipanga kutembelea Mbuga za wanyama za Mikumi tarehe 02 Machi na tayari zoezi hilo limeshafanyika, 05 Machi limefanyika kongamano la wanawake na tarehe 06 Machi ni zoezi la upandaji wa miti kwenye Mituo cha Afya Mkoga kwa lengo la kutunza Mazingira.
"Leo wanawake wote wa Manispaa tumeungana pamoja ili kuboresha Mazingira kama kauli ya Mama Samia Sulluhu inavyosema kuwa kila iitwapo leo tukumbuke kupanda Miti. Lakini pia tunapopanda miti ya matunda ili wagonjwa waweze kula na kuboresha afya". Amesema Mtamakaya
Aidha, Afisa Misitu wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Ndg, Enock Changime amesema yeye kama Mtaalamu wa Misitu ameshiriki kwenye zoezi hilo ili kuweza kuwaongoza na kuwasaidia kina mama na hatimaye zoezi hilo liende vizuri.
Pia, Akitoa elimu ya upandaji miti kwa wakina Mama amesema kuwa miti ina faida nyingi ambapo itanufaisha wagonjwa na kuboresha Mazingira kiujumla.
"Faida ya upandaji wa miti ambayo tumepanda eneo hili, kwanza Kuna faida za moja kwa moja ambazo wagonjwa watakaokuja eneo hili watanufaika kwa maana ya matunda, pili wataweza kupata kivuli na tatu wataweza kupata hewa safi", Amesema Changime.
Pia, amesema kuwa wagonjwa watakaofika eneo hilo watapewa miche ya miti kwa ajili ya kupanda kwenye maeneo yao. Mbali na hilo, amewashauri wananchi wajitokeze kwa wingi kwenye mazoezi mengine kama hayo.
Kwa upande wake, Afisa Afya kata ya Isakalilo Ndg, Matilda Kasanga ameushukuru uongozi wa Manispaa ya Iringa hasa Serikali ya Mama Samia kwa kuweza kujenga kituo cha afya cha Mkoga kwani kitasaidia kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo hususani kina mama, wajawazito na watoto ambao ni walengwa wakuu.
Kasanga amemshukuru Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa kwa kuweza kuwapatia Miti katika Kituo hicho cha afya ili kuboresha Mazingira na ametoa wito kwa wananchi wa eneo hilo watunze kituo hicho.
Naye mkazi wa kata hiyo, Ndg, Twina Nyaulembo ameishukuru Serikali kwa kupeleka kituo cha Afya kwenye Kata hiyo. Pia amewapongeza wanawake kwa upandaji wa Miti na ataendelea kuelimisha na kuhamasisha jamii ili kila mmoja aone umuhimu wa kupanda miti.
Maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani hufanyika Tar 08 Machi kila mwaka, ambapo wanawake wa Manispaa ya Iringa wataungana na Mkoa kuadhimisha sherehe hizo kimkoa katika uwanja wa Samora
Kauli mbiu ya mwaka huu inasema, "Wekeza kwa Mwanamke Kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii".
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa