Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete ametoa rai kwa Maafisa Utawala na Rasilimali watu kushughulikia kero za watumishi na kuitisha mikutano ya ndani ili kupata majibu ya changamoto zilizopo ndani ya Mkoa.
Mhe. Kikwete amesema hayo akiwa katika ukumbi wa “Siasa ni Kilimo” wakati akizungumza na watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa katika ziara yake Mkoani humo na kutoa fursa ya watumishi kueleza changamamoto na kero mbalimbali wanazokumbana nazo katika utumishi wa umma na maeneo yao ya kazi kwa ujumla.
“Maafisa Utawala na Rasilimali watu muwe na utaratibu wa kusikiliza kero za watumishi na kuzitatua kwa manufaa ya taifa la kesho, na pia natoa rai yangu mfanye mikutano ya ndani kwani hii inasaidia kutatua changamoto, msisubiri mpaka aje Waziri au Naibu Waziri ndipo mzungumze na watumishi, itisheni mikutano yenu.” Amesema Mhe. Kikwete
Mhe. Kikwete ametoa ufafanuzi kwa watumishi juu ya hoja zilizoibuliwa na kuacha maagizo kwa Maafisa Utawala na Rasilimali watu kushughulikia stahiki za watumishi kama vile Nyongeza ya mshahara, Kupandishwa madaraja, Pesa ya kujikimu kwa watumishi wapya, Malipo ya likizo, Matibabu, Uhamisho, Malipo ya pensheni kwa wastaafu pamoja na vitendea kazi katika ofisi.
Aidha Mhe. Kikwete ameiagiza Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kuwapa barua vijana 37 kati ya 47 waliokuwa wakijitolea kukaimu nafasi ya Utendaji wa Mitaa na kufanya usaili Septemba 2023.
Mkutano huu unalengo la kushughulikia masuala ya utumishi wa umma mkoani Iringa na umehudhuriwa na Katibu Tawala Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Katibu Tawala Wilaya, Waheshimiwa Wabunge, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Viongozi wa TASAF kutoka Makao Makuu na watumishi.
Iringa Municipal Council
Sanduku la Posta: 162
Telephone: +255-2702647
Mobile: 255-2702647
Email: md@iringamc.go.tz
hakimiliki@2017Iringa Manispaa haki zote zimehifadhiwa